Mtwara. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred ametangaza kuanza kwa minada ya korosho ghafi nchini ifikapo Oktoba 11, 2024.
Alfred amebainisha hayo leo Septemba 13, 2024 mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Seleman Serera mkoani Mtwara wakati wa kikao cha kujadili mfumo wa ununuazi wa korosho.
Amesema minada hiyo inatarajia kuanza huku wakulima wakiwa wamepunguziwa mzigo wa tozo, hivyo wakitarajia kulipwa fedha zao bila makato.
Mkurugenzi huyo amesema katika msimu wa uuzaji wa korosho ghafi, tozo zote zimewekwa kwa mnunuzi na bei itakayotajwa kwenye mnada ndiyo fedha ambayo mkulima atalipwa.
Amesema mkulima atakatwa fedha ya usafiri pekee, tozo zote zitalipwa na mnunuzi, hili kwetu ni jambo jipya ambalo tunapenda mkulima afalihamu.
“Msimu huu tozo zote zimewekwa kwa mnunuzi, bei itakayotajwa kwenye mnada ni pesa ambazo mkulima analipwa, atakatwa pesa ya usafiri tu,” amesema Alfred.
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Benson Ndiege amesema katika msimu huu, mizani ya kisasa itatumika ambapo mkulima atapata fursa ya kupokea taarifa ya mzigo aliofikisha katika chama cha msingi.
“Tunatarajia mizani itatumia mwishoni mwa mwezi huu, lazima mizani hii ya kidigitali itumike ipasavyo, asiyetumia chukueni hatua. Inachukua taarifa za mkulima ikiwemo uzito na taarifa anapata hadi kwenye simu yake ili kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa usahihi na uwazi.
“Simamieni matumizi ya mizani hii katika msimu huu kwa kuwa wapo baadhi viongozi wa vyama vya ushirika ambao hawajawa tayari kutumia mizani hii au pengine wanaiweka pembeni,” amesema Ndiege.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfumo wa Mauzo wa Kielektroniki (TMX), Godfrey Malekano amesema katika msimu wa uuzaji wa korosho wa 2024/25, wameboresha mfumo wa uuzaji wa korosho kidigitali.
“Tunahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau wote muhimu katika msimu huu wa uuzaji wa korosho, kwa sasa tunaboresha mfumo huo ambapo kwa sasa tumepanga kukutana na wadau ili kuangalia namna bora ya kuutumia mfumo huu wa TMX,” amesema Malekano.
Serera ameviagiza vyama vya ushirika kuwa chachu ya mabadiliko kwa wakulima kwa kusimamia ununuzi wa korosho na utaraibu mzima wa minada wa mwaka 2024/25.