WAKATI maafande wa Zimamoto na JKU wakishuka uwanjani jioni ya leo katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar, juzi Kipanga na Uhamiaji zilipata aibu baada ya kufungwa, huku Mlandege ikibanwa na wageni Junguni nyumbani, kwenye Uwanja wa Amaan B, mjini Unguja.
Kipanga ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Gombani, ilifumuliwa na Mwenge mabao 2-1, huku Uhamiaji ikinyooshwa na mabingwa wa Kombe wa Shirikisho, Chipukizi mabao 2-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan A na kubadilisha hali ya msimamo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya pili kwa sasa.
Katika mechi ya Pemba, wenyeji Mwenge ilipata ushindi kwa mabao ya jioni likiwamo la kujifunga la beki wa Kipanga, Onesmo Timoth Haule dakika ya 80, likiwa la kusawazisha baada ya awali Aqram Ahmed Zubeir kuwatanguliza wageni kwa bao la dakika ya 60.
Dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho, Ali Omar Ali alifunga bao la ushindi la wenyeji na kuipa ushindi wa kwanza katika ligi hiyo iliyoanza Septemba 6 na kuifanya ifikishe pointi tatu na kushika nafasi ya tisa kutoka ya 13 iliyokuwapo awali (hii kabla ya mechi ya jana kati ya KMKM na Muembe Makumbi City).
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Mwenge, Mustafa Hassan Suleiman alisema kupoteza mchezo wa kwanza mbele ya KVZ uliliamsha benchi la ufundi na kufanya maboresho na mikakati ya kuona sasa kila mchezo wanashinda na wanashukuru wameanza mbele ya Kipanga.
“Tunashukuru kwa kuvuna pointi tatu, tumepoteza mchezo wa kwanza tukaamua kakaa chini kurekebisha makosa yetu tukashinda mchezo huu na mafanikio haya yatakuwa enndelevu,” alisema Mustafa, huku Kocha wa Kipanga, Mashaka Ramadhani aliwataka mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuwa na subra kwani makosa yalojitokeza watakwenda kuyafanyia kazi.
Alisema baada ya bao la kusawazisha walilofunga Vijana wake walitoka mchezoni, kabla ya kufungwa lingine, hivyo watajipanga kwa michezo mengine.
“Tukubali tumefungwa lakini tayari mapungufu yaliyojitokeza tutakwenda kuyafanyia kazi ili tufanye vizuri kwenye mchezo unaofuata. Niwaombe mashabiki watulie, bado ni mapema tutashida michezo mengine,” alisema Mashaka.
Kwenye Uwanja wa Amaan A, mabao mawili kila kipindi la
Nunu Mwarabu dakika ya 34 na Mundhir Iman Moh’d dakika ya 66 yaliifanya Chipukizi ipande hadi nafasi ya kwanza na kuishusha KVZ, licha ya kulingana pointi nne na zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Matokeo hayo yameifanya Uhamiaji iliyotolewa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kipigio cha mabao 5-1 na Al Ahli Tripoli ya Libya inayocheza na Simba kesho katika mechi za raundi ya pili, isaliwe na pointi tatu na kuporomoka kutoka nafasi ya tatu hadi ya nane.
Kwenye Uwanja wa Amaan B, Mlandege iliendelea kusuasua ikipata suluhu ya pili mfululizo baada ya kubanwa na wageni wa ligi hiyo Junguni ya Pemba, baada ya awali kulazimishwa suluhu na Chipukizi pia ya Pemba na sasa ina pointi mbili,huku Junguni ikiandikisha pointi ya kwanza baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1 dhidi ya Uhamiaji ugenini.
Ligi hiyo itaendelea leo Jumamosi kwa mchezo mmoja wa kukata na shoka unaozikutanisha Zimamoto dhidi ya JKU ambao ni watetezi wa taji hilo.
Katika mechi za kwanza zilizopita kwa timu hizo, JKU ilianza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wageni wa ligi hiyo Inter Zanzibar ya Unguja, huku Zimamoto ikizamishwa mabao 2-1 na Malindi, hivyo kufanya mchezo huo wa leo kuwa mgumu kutabirika.
Msimu uliopita timu hizo hazikuchekana kwani kila moja ilishinda mechi ya nyumbani, JKU ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 mchezo uliopigwa Sept 29, 2023 kabla ya Zimamoto kujibu mapigo kwa kuwafumua 4-0 ziliporudiana Feb 23, 2024.