Geita. Vilio vimetawala mazishi ya Theresia John (18), mwanafunzi wa kidato cha nne aliyepoteza maisha kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwao, Kijiji cha Lulembela wilayani Mbogwe, wakati wa vurugu zilizotokea baina ya askari polisi na wananchi.
Vurugu hizo zilitokana na kundi la wananchi waliofika kituo cha polisi kijijini hapo wakishinikiza polisi iwakabidhi wanaume wawili waliodhaniwa kuwa wezi wa watoto ili wawaue.
Kufuatia hali hiyo, polisi walitumia mabomu ya machoni na risasi za moto na Theresia aliyekuwa nyumbani kwao, alipigwa risasi na kufariki dunia na mwanaume mwingine ambaye hakutambulika, naye alipoteza maisha.
Mazishi hayo yamefanyika leo Septemba 13, 2024 na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa.
Akitoa salamu za pole, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Serikali haitatulia hadi pale waliohusika na vurugu hizo watakapokamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Huyu ametangulia mbele za haki kwa sababu ya watu tu kwa malengo yao wanayoyajua, askari wako kazini mnapovamia kituo huwezi kujua nani mkweli na nani ana haki. Katika kujibizana na askari lolote linaweza kutokea, niwasihi sana ndugu zangu kuna mambo ya kuchezea lakini sio kituo cha polisi,” amesema Shigella.
Shigella amesema ana uhakika watu walioongoza vurugu hizo ni wakazi wa eneo la Lulembela na wanafahamika, hivyo wananchi wawafichue kwa kuwa ni watu hatari katika jamii.
“Serikali tumesikitishwa na kifo cha mtoto na kijana mwingine, tupo kazini tutawatafuta na kuwasaka wote waliohusika.
“Wala msitafute mchawi kuwa fulani ndio ametutaja, vyombo vyetu vina macho ya ziada, msimhukumu mtendaji wa kijiji wala mwenyekiti wa kijiji, wala diwani hawahusiki, hawa waliofanya vurugu watatafutwa hadi wapatikane na sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Diwani wa Kata ya Lulembela, Deus Lyankando amesema tukio hilo ni baya na la kutisha lililosababisha kifo cha mtu asiye na hatia.
“Wananchi wameponda kituo mawe na yale mawe tunajaza trekta, tunapata wapi uwezo wa kufuata wenye bunduki kwa mawe? Nawaomba sana mtii sheria bila shuruti, watu kwenye eneo letu wamekimbia,” amesema.
Amesema kutokana na vurugu zilizotokea kituo kimefungwa na askari wamerudi makao makuu na hivyo ameiomba Serikali kurudisha kituo kwa ajili ya ulinzi na kuomba kituo kinachojengwa kikamilike ili kisiendelee kukaa kwenye makazi ya watu.