Dodoma. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (Tira) kwa kushirikiana na wadau wa bima imeshauriwa kutoa elimu ya bima kwa wananchi hasa yanapotokea majanga kwa wateja wao, ili wananchi wengi wajue umuhimu wa kukatia bima shughuli zao za kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa, Septemba 13, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja kwenye matembezi ya kuadhimisha Siku ya Bima nchini, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.
Mayanja amesema ni Watanzania wachache wenye uelewa kuhusu huduma za bima lakini kundi kubwa halina elimu, hivyo yanapotokea majanga kwa wateja wao wenye bima, watumie fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi.
“Nina fahamu Tira mnafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, lakini ukiangalia namna nchi yetu na wananchi wake wanavyopiga hatua za kimaendeleo kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi, bado kuna changamoto za wadau kutokatia bima shughuli wanazozifanya,” amesema Mayanja.
Amezitaka taasisi za bima nchini ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha Watanzania walio wengi wanapata elimu ya bima ambapo wakipata elimu ya kutosha kwa fursa zilizopo watachukua hatua maana.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT), Magreth Kongo amesema suala la bima ni la kila Mtanzania kwa sababu kila mwananchi anahitaji huduma za bima ili aweze kupata msaada anapopatwa na majanga mbalimbali, zikiwemo ajali, magonjwa na moto
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango amewataka Watanzania kukatia bima shughuli zao za kiuchumi ili yanapotokea majanga wasitetereke bali waweze kuinuka na kuendelea.
“Tunaona mara nyingi masoko yanashika moto na kuteketeza mali zote lakini kama umekatia biashara yako bima baada ya muda unarudi kuendelea na biashara yako, tofauti na yule asiye na bima, ambapyo hupoteza kila kitu na kulazimika kuanza upya,” amesema Shango.
Aidha taasisi hizo za bima nchini zimetoa msaada wa kuchangia damu kwenye kituo cha damu salama kilichopo Dodoma na msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh15 milioni kwenye wodi ya watoto njiti iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.