Geita. Shughuli za kiuchumi katika eneo la Lulembela, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita zimeanza kurejea baada ya wafanyabiashara kufungua maduka yao.
Biashara katika eneo hilo zilisimama kuanzia Septemba 11, 2024 hadi leo Septemba 13, 2024 walipoanza kufungua maduka, licha ya kuwa bado wateja wanasuasua kwa sababu ya hofu ya kukamatwa.
Wafanyabiashara walifunga maduka yao baada ya kutokea vurugu zilizotokana na baada ya wananchi kuvamia kituo cha polisi Lulembela kuwatoa wanaume wawili waliokuwa wamebeba watoto, wakidaniwa isivyo kuwa ni wezi wa watoto na hivyo kukabiliana na polisi.
Kufuatia vurugu hizo, watu wawili walipoteza maisha akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Lulembelela ambaye alifikwa na mauti akiwa nyumbani kwao akijaribu joho la mahafali.
Lucas Mashine, mfanyabiashara katika eneo hilo, amesema kwa sasa amani imerejea na maisha yanaendelea lakini mwitikio wa wateja ni mdogo kutokana na wananchi kuwa na hofu.
“Hapa unaona watu wamekuja wanapooza koo, hawa ni wageni lakini bado watu wana wasiwasi, wenyeji bado wana hofu lakini hali ikiendelea hivi maisha yatarudi kama zamani.
Kwa upande wake, Rehema Suleiman, mfanyabishara wa saloon, amesema licha ya kuwa, jana jioni (Septemba 12, 2024) alifungua lakini hakupata mteja hata mmoja kwa sababu watu wakiona gari la polisi wanakimbia, hivyo kufanya watu waishi kwa hofu.
“Tunaweza kusema shughuli za kiuchumi zilishuka hapa, watu hata kusimama barabarani ilikuwa vigumu, hali ya hapa ilikuwa ya taharuki. Kwa leo licha ya kuwa hali haijawa shwari lakini angalau huduma zipo, siyo kama jana,” amesema.