SMZ yatekeleza malipo ya fidia kazini, 81 wanufaika

Unguja. Mwaka mmoja tangu Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ulipoanzisha skimu ya fao la fidia kwa wafanyakazi wanaopata majanga kazini, jumla ya wafanyakazi 81 wamenufaika.

Skimu ya fidia ya ZSSF imeanzishwa mwaka 2023 kutokana na marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, Na.2 ya mwaka 2005 na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi namba 15 ya mwaka 1986 kupitia sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba tano na 10 ya mwaka 2022 ambayo ilifanya fidia ya ajali kazini kuwa moja ya mafao yanayolipwa na ZSSF.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema hayo leo Septemba 13, 2024 katika Mkutano wa 16 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.

Dk Saada alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman aliyetaka kufahamu lini skimu hiyo itaanza kutekelezwa ili kuwanufaisha wafanyakazi wanaopata madhila hayo na katika kuipunguzia mzigo ZSSF kwa nini Serikali haikuona haja ya kuja na chombo kingine kitakachosimamia jambo hili.

Akijibu swali hilo, Dk Saada amesema tayari skimu hiyo imeshaanza kutekelezwa tangu Julai mwaka 2023 na hadi Juni, 2024 watu 81 wameshalipwa Sh260.420 milioni.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Agosti, skimu ya fidia imeshalipa mafao ya kuumia kazi kwa wafanyakazi wanane walioumia kazini na jumla ya Sh5.869 milioni zimetumika kulipa mafao hayo,” amesema.

Kuhusu kuunda chombo kingine kutekeleza majukumu hayo badala ya kuiongezea majukumu ZSSF, Dk Saada amesema mwaka 2022 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilifanya maamuzi ya kutaka ZSSF kulipa fao la kuumia kazini na haikuona haja ya kuunda chombo mahususi kwa ajili hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

“Fao la kuumia kazini ni moja ya mafao ya hifadhi ya jamii yanayotolewa na ZSSF hivyo, kuitaka ZSSF kuongeza fao hilo siyo mzigo na ni njia rahisi ya kuhahikisha fao hilo linalipwa kwa ufanisi,” amesema.

Amesema ZSSF una uzoefu mkubwa na wa muda mrefu wa kulipa mafao ya hifadhi ya jamii, hivyo uzoefu huo umerahisisha ulipaji wa fao la kuumia kazini kwa weledi na kupunguza gharama ya kuanzisha chombo kipya mahususi kwa ajili ya fao moja tu.

Kupitia marekebisho ya sheria namba 10 ya mwaka 2022 ilifanya marekebisho ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi namba 15 ya mwaka 2022 na kuipa mamlaka ZSSF kulipa mafao ya kuumia kazini kwa wafanyakazi wote wa sekta ya umma na sekta binafsi ambao ni wanachama wa ZSSF.

Kutokana na marekebisho hayo ya sheria waajiri wote wanachangia asilimia moja katika skimu ya fidia ya ZSSF kwa ajili ya kulipia fao la kuumia kazini.

Related Posts