ZFDA yanasa bidhaa za vyakula zilizoisha muda wa matumizi

Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi umekamata bidhaa za vyakula na vipodozi zilizokwisha muda wa matumizi katika maduka yaliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Bidhaa hizo ni mafuta ya kula tani moja, bia, maharage na mahindi ya kwenye makopo, maziwa, na tambi.

Bidhaa nyingine ni sabuni na vipodozi vilivyopatikana katika maduka yaliyopo maeneo ya darajani, Wilaya ya Mjini.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Septemba 13, 2024 katika ofisi za ZFDA Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula na Ufanisi, Dk Khamis Ali Omar amesema kutokana na ukaguzi wamebaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaoendesha shughuli hizo bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Amesema bidhaa nyingi zilizokamatwa katika ukaguzi muda wake wa matumizi umekwisha na nyingine zilipigwa marufuku nchini kutokana na kuwa na viambata vya sumu, hivyo kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya udanganyifu kwa kubadilisha tarehe ya muda wa matumizi.

“Baadhi ya bidhaa zinaelekeza ukitaka maelezo ya muda wa matumizi yapo chini ya bidhaa hii, ukiangalia utakuta michubuko inayoashiria maelezo hayo yamefutwa, badala yake unakutana na kikaratasi chembamba cha maelezo ya muda wa matumizi karibu na mfuniko wa bidhaa,” amesema.

Dk Khamis amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuangalia uhalali wa wafanyabiashara na usalama wa bidhaa, na kila wanapofanya ukaguzi hukutana na matukio kama hayo.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi kwani jambo hilo husababisha athari kwa watumiaji.

Baadhi ya wananchi waliozungumzia hatua hiyo, wamesema mamlaka inatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua kali kwa wanaobainika kwa kuwa bidhaa hizo ni hatari.

“Huenda hata watu wakatapa magonjwa kwa sababu ya vitu kama hivi, wanaobainika kufanya udanganyifu huu wanapaswa kuchukuliwa hatua kali iwe fundisho kwa wengine,” amesema Nasrat Awadh Mussa, mkazi wa Tomondo.

Related Posts