WADAU WAITWA KUSAIDIA WAZEE – Mzalendo

Na WMJJWM, Dar Es Salaam

Wadau mbalimbali wameombwa kujitokeza kuunga mkono ajenda za kundi la wazee ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wazee.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo Septemba 13, 2024 jijini Dar Es Salaam, wakati akifunga kongamano la mwaka la wazee sambamba na uzinduzi wa Shirika la Helpage Tanzania.

Waziri Dkt. Gwajima amesema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha ustawi wa wazee, bado kuna baadhi ya changamoto ikiwemo idadi ndogo ya Asasi za Kiraia (CSOs) zinazojishughulisha na masuala ya wazee pamoja na zilizopo kukabiliwa na uchache wa rasilimali.

“Kuna changamoto za mwitikio mdogo wa baadhi ya wadau kwenye kuunga mkono ajenda za kundi la wazee ukilinganisha na ajenda za makundi mengine mathalani, Dira na misheni za baadhi ya wadau mara nyingi zinajikita katika maeneo maalum, hasa mikoa na wilaya walipo”. Amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto za Wazee nchini ikiwemo za kiuchumi kwani zaidi ya asilimia 70 ya wazee wanaojishughulisha kiuchumi, mara nyingi hufanya kazi katika sekta zisizo na tija na kushindwa kujikimu kimaisha.

Ameongeza kuwa, katika hali ya uhaba wa taasisi zinazojishughulisha na masuala ya wazee nchini, jukumu la taasisi za dini lina umuhimu mkubwa na zina mchango mkubwa katika kuimarisha huduma kwa wazee na kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa.

Amelipongeza shirika la Helpage Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuchochea maendeleo ya Wazee na kuleta matokeo makubwa na kwamba, uzinduzi wake umekuja katika wakati muafaka kwani bado kuna mahitaji makubwa ya wazee yanayochangiwa na mabadiliko ya kiutamaduni, kiuchumi, kiteknolojia, kijamii na afya.

Kuhusu kongamano hilo, Waziri Dkt. Gwajima amesema anaamini majadiliano ya wazee hao yatakuwa msingi wa kuainisha juhudi za kitaifa kuelekea mwaka 2050 kwa kutambua mambo mengi yanayoweza kusaidia kufikia malengo ya mifumo ya kisheria, teknolojia na taasisi za kidini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mendelwo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushikiriana na shirika hilo pamoja na wadau wengine inaendelea na juhudi kuhakikisha haki na ustawi wa wazee unafikiwa hasa Sera, kanuni na sheria za kuwalinda wazee.

Kwa upande wao baadhi ywa wazee walioshiriki kongamano hilo akiwemo Salama Ahmed Kombo na Katibu wa Baraza la Wazee Taifa
Anderson Lyimo wameishukuru Serikali na wadau wanaoshughulika na masuala ya wazee na kuomba maazimio waliyojiwekea yafanyiwe kazi hasa katika kuwasihi wadau kujenga uwelewa kwa jamii kuhusu nafasi ya wazee na kuwaenzi.

Related Posts