Dar es Salaam. Miaka kadhaa iliyopita upatikanaji wa sukari Tanzania ilikuwa miongoni mwa masuala yaliyoitatiza Serikali kuhamasisha uwekezaji mpya ili kuhakikisha uzalishaji unatosheleza mahitaji.
Takwimu zilizopo zinaonyesha mahitaji ya sukari kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani ni tani zaidi ya 650,000 na uzalishaji wa ndani haukidhi mahitaji.
Mikate, vinywaji baridi, migahawa na baadhi ya vyakula, vyote vinategemea sukari, hivyo kuifanya kuwa rasilimali muhimu.
Miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa sukari nchini ni kampuni ya Kitanzania iliyoanzishwa zaidi ya miongo sita iliyopita inayozalisha tani 126,000 kila mwaka.
Tangu mwaka 1960, Kampuni ya Sukari Kilombero imekuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo Tanzania.
Pamoja na Illovo Sugar kumiliki hisa asilimia 75 na Serikali ya Tanzania asilimia 25, kampuni hii inayojulikana kwa chapa maarufu ya ‘Bwana Sukari’ imejiimarisha vilivyo.
Baada ya mafanikio ya nusu karne, Kampuni ya Sukari Kilombero ilichukua hatua kubwa ya upanuzi wa kiwanda cha K4.
Agosti 4, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka jiwe la msingi la mradi huo, Kampuni ya Sukari ya Kilombero ikitangaza asilimia 90 ya mradi huo unaohusisha ujenzi wa kiwanda kipya na cha kisasa cha K4 upo katika hatua za mwisho.
Mradi huu mkubwa wa K4 unaotekelezwa mkoani Morogoro unatarajiwa kuleta mabadiliko, ukitengeneza fursa za ajira kwa wakazi wa Kilombero na maeneo ya jirani.
Idadi ya wakulima wa miwa inatarajiwa kuongezeka kutoka 8,000 waliopo sasa na kufikia kati ya 14,000 na 16,000 baada ya uzinduzi kufanyika.
Katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa K4 hivi karibuni, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Suleimani Jafo alisisitiza, “mradi huu unaonyesha kujitoa kwenu kwa dhati kwa muda mrefu katika kuchochea ukuaji wa viwanda na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za Taifa letu.”
Kwa mujibu wa Kampuni ya Sukari Kilombero na wataalamu wa viwanda, mradi wa K4 unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa, kwani uwezo wa kiwanda kutengeneza sukari unatarajiwa kuongezeka maradufu.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza tani 144,000 za sukari kila mwaka, hivyo kuongeza uzalishaji wa jumla kutoka tani 126,000 hadi tani 271,000 kwa mwaka.
Akihutubia wakati wa uwekaji jiwe la msingi la mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero, Guy Williams alisisitiza kuhusu mchango mkubwa wa mradi huo mpya kwa uchumi wa Tanzania. Alisema, “mradi huu utaifanya Tanzania kujitosheleza kwa sukari na kuokoa kati ya Dola 70 milioni hadi Dola 90 milioni za Marekani, kutokana na kutokuhitaji tena kuagiza sukari nje ya nchi.”
Siyo tu uzalishaji wa sukari unaotarajiwa kuongezeka baada ya uzinduzi wa mradi wa K4, kampuni hiyo ikiwa miongoni mwa wauzaji wakuu wa ethanol barani Afrika, pamoja na Afrika Kusini, Eswatini na Uganda, uzalishaji na usafirishaji wa kemikali hiyo nchini unatarajiwa kuongezeka zaidi baada ya kukamilika kwa mradi wa K4.
Hivi sasa Tanzania inauza ethanol Uswisi, Uholanzi na Kenya. Mradi wa K4 unatarajiwa kupanua wigo huo na kuongeza idadi ya nchi zinazoagiza ethanol kutoka Tanzania.
Kiwanda kipya kitazidisha uzalishaji wa ethanol kwa kilolita 4,000 zaidi, na kuleta uzalishaji wa jumla wa kila mwaka hadi kilolita 16,000.
Ongezeko hilo litawezesha kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya pombe inayoweza kunyweka, ndani ya nchi na kuuza katika soko la nje la Afrika Mashariki, kuhakikisha kanda inabaki mstari wa mbele kwenye maendeleo ya viwanda.