Morogoro. Wakati uchaguzi wa serikali za mitaa ukitarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, watu wenye ulemavu wameiomba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuwapa nafasi ya kushiriki kusimamia uchaguzi kama ilivyo kwa watu wengine.
Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Wilaya ya Morogoro, Aisha Abdalah amesema ili watu wenye ulemavu huo waweze kushiriki kusimamia uchaguzi, chama hicho kimepeleka barua kwa msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Morogoro kuomba kufanya kazi hiyo.
“Uwezo wa kusimamia uchaguzi tunao kama walionao watu wengine, tukisimamia tutaweza kuwasaidia hata na wenzetu wengine wenye ulemavu wa aina hii watakapokuja kupiga kura na kuhitaji msaada,” amesema Abdalah.
Amesema chama hicho kimeendelea kutoa hamasa kwa watu wenye ulemavu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za mitaa.
Ameiomba INEC kuzingatia watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu hasa wakati wa kutoa matangazo kwenye runinga na mikutano ya hadhara, yanayohusu elimu ya mpigakura ili waelewe kinachotangazwa.
“Kituo fulani cha televisheni au hizi habari za kwenye mitandao ya kijamii kinaweza ikaweka tangazo linalohusu masuala ya uchaguzi inaweza ikawa elimu kwa mpigakura. Sasa sisi wenye ulemavu wa kutosikia tunajikuta tunapitwa na elimu hiyo kwa sababu tu hakuna mtu wa kutafsiri kwa lugha ya alama, hivyo tunaomba wakati wa kutoa elimu ya mpigakura inayotolewa kwenye vituo vya televisheni, awepo mtu wa kutafsiri kwa lugha ya alama ili na sisi tuweze kupata elimu hiyo.
Pia ameomba vyama vya siasa kuweka wakalimani kwenye mikutano ya kampeni ili kutafsiri kwa lugha ya alama kuwezesha wenye ulemavu wa kutosikia kujua sera za wagombea kutoka kwenye vyama hivyo vya siasa.
“Kwenye chaguzi zilizopita tulikuwa tunakwenda kwenye mikutano ya kampeni lakini hatusikii kinachosemwa na wagombea, tukienda tunaangalia wasanii tu wanavyocheza pale jukwaani na kuwaona wagombea lakini sera wanazonadi hatusikii, sasa kama kutakuwa na wakalimani wa lugha ya alama itatusaidia kujua sera za wagombea na hata siku ya uchaguzi tungekuwa tunapiga kura kwa kuwa tunajua mgombea huyu kaahidi nini tofauti na ilivyo sasa tunapiga kura kwa hisia tu na kwa kumpenda mgombea kwa mwonekano wake.
Issa Kipigo, mwenye ualbino amesema watu wenye ulemavu wana haki ya kushiriki kwenye mambo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo kushiriki kwenye uchaguzi, hivyo ameomba INEC kuwaamini na kuwapa nafasi ya kusimamia uchaguzi.
Kipigo anasema kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ni muhimu kupata nafasi ya kushiriki kusimamia uchaguzi waweze kutoa msaada kwa wenzao watakaofika kwenye vituo vya uchaguzi.
“Sisi ni watu tunaohitaji uangalizi mkubwa, hasa kwenye chaguzi, hatutakiwi kukaa kwenye foleni na kupigwa na jua, pia kwenye mwanga wa jua tunasumbuliwa na macho hivyo mtu asiyekuwa na ulemavu huu anaweza asijue mahitaji yetu lakini sisi tukiwepo kwenye usimamizi wa uchaguzi tutaweza kuwasaidia wenzetu,” amesema.
Amesema suala la unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu linapaswa kukemewa na kuwekezwa nguvu za kisheria, ili watu wenye ulemavu waweze kupata haki sawa na watu wengine ikiwemo haki ya kuchagua kiongozi au kuchaguliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa mujibu wa Kipigo, katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye siasa au Serikali zilizowahi kushikwa na watu wenye ulemavu wameonekana kuzitendea haki nafasi hizo kwa kutekeleza vyema majukumu yao na hivyo kuaminiwa na wananchi na hata Rais.
Ameiomba Serikali kuwaamini na kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali ya kitaifa.
Kibena Iddy, mlemavu wa viungo amesema suala la kusimamia uchaguzi kwenye vituo halihitaji elimu kubwa ya chuo kikuu wala nguvu kubwa, hivyo wapo watu wenye ulemavu ambao wanaweza kufanya shughuli ndogondogo kwenye vituo vya kupigia kura.
“Kwenye vituo vya kupigia kura zipo shughuli kama za kuwapanga watu kwenye mistari kupiga kura, kugonga mihuri kwenye karatasi za kupigia kura, kubeba masanduku ya kupigia kura, kubandika matangazo na shughuli nyingine wanazostahili kulingana na ulemavu wao,” amesema Iddy.
Ameiomba INEC kuona umuhimu wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa na hata uchaguzi mkuu wa mwakani.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Solomon Kasaba akizungumzia mipango yao ya kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wenye ulemavu wa kutosikia, amesema wanaendelea kuangalia namna ya kufikisha sera zao kwa makundi hayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani hapa, Abed Mlapakolo amesema hakina bajeti kwa ajili ya kuajiri wakalimani wa lugha ya alama, japokuwa mara kadhaa wamekuwa wakijadili kupitia vikao namna ya kulifikia kundi hilo na kulipa haki yake ya kikatiba.
“Ni kweli watu wenye ulemavu ni binadamu kama wengine na wana haki sawa lakini kuna wakati tunashindwa kuyafikia makundi haya kwa sababu ya bajeti. Chama hakina uwezo wa kuajiri wakalimani ili wawepo kwenye mikutano yote ya kampeni, isipokuwa tunaweza kufanikisha hili kwa kushirikiana na Serikali kama ambavyo tumefanikiwa katika kuyapa haki makundi mengine wakiwemo wafungwa magerezani,” amesema Mlapakolo.
Amesema wanaendelea kulisemea hilo kwa Serikali kwa sababu kwa kuwa makundi maalumu yana haki ya kuchagua kiongozi kulingana na sera wanazozisikia na si kubahatisha kama wanavyofanya sasa.
“Tutahakikisha tunalisemea hili ili lifanikiwe kama lilivyofanikiwa la watu wenye ulemavu wa macho kupata maandishi ya nukta nundu wanazotumia kupigia kura,” amesema.
Mlapakolo amesema pamoja na mikakati mizuri ya kuwashirikisha wenye ulemavu wa kutosikia lakini changamoto iliyopo ni wataalamu wachache wa lugha ya alama watakaoweza kukidhi mahitaji hasa kwenye kutafsiri sera za wagombea kwenye mikutano ya siasa, kampeni na hata siku ya kupiga kura.
Ameiomba Serikali kuhimiza wananchi kujifunza lugha ya alama ili nchi iwe na wataalamu wa kutosha watakaoweza kuwasaidia wenye ulemavu wakati wa chaguzi lakini pia wanapotaka kupata huduma za kisheria, matibabu na nyingine za kibinadamu.
Wakati hayo yakielezwa na watu wenye ulemavu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imetoa mwongozo wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Mwongozo huo hauwazuii watu wenye ulemavu kusimamia uchaguzi.
Kuhusu uteuzi wa msimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi mwongozo unaeleza ifuatavyo:
‘’Kutakuwa na msimamizi wa uchaguzi, atakayeteuliwa kusimamia uchaguzi; kutakuwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi kwa kila mtaa, kitongoji na kijiji watakaoteuliwa na msimamizi wa uchaguzi.
Wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi watakaoteuliwa wanatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
Wasiwe na dhamana au uongozi katika chama chochote cha siasa, wawe ni watumishi katika utumishi wa umma, na wawe waadilifu.
Mbali na hayo, kanuni zinazosimamia uchaguzi huo zinatoa nafasi ya usaidizi kwa wapigakura wenye changamoto mbalimbali.
Kanuni zinaeleza mpigakura ambaye kwa sababu ya ulemavu wa macho au
ulemavu mwingine wowote; au hajui kusoma na kuandika, anaweza kumwomba mtu yeyote kumsaidia kupiga kura.
Kanuni zinaeleza, isipokuwa mpigakura huyo hataruhusiwa kuomba usaidizi wa msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, mgombea au wakala wake.
Inaelezwa bila kuathiri masharti ya kanuni, mtu mmoja hataruhusiwa kumsaidia mpigakura zaidi ya mmoja.