Tuzo yampa nguvu staa Mashujaa

ABDULRAHMAN Mussa ambaye anatumika kama beki wa kulia ndani ya kikosi cha Mashujaa, amesema tuzo aliyoipata katika mchezo dhidi ya Coastal Union imempa nguvu mpya ya kuendelea kupambana.

Mussa ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo mshambuliaji, juzi Ijumaa alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam na kukabidhiwa tuzo zinazotolewa na mdhamini mkuu wa ligi hiyo.

Katika mchezo huo ambao Coastal walikuwa wenyeji, walijikuta wakipoteza kwa bao la Crispin Ngushi dakika ya 14, Mussa akitoa asisti ya bao.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mussa alisema hiyo ni mara yake ya kwanza kuchukua tuzo ya aina hiyo, hivyo anaona imemfungulia milango ya kuzichukua nyingine zaidi katika michezo ijayo.

“Nina furaha kubwa sana kwani hii ni mara ya kwanza kuchukua tuzo ya namna hii. Kwangu ni tuzo kubwa.  Namshukuru Mungu, nazidi kumuomba niendelee kufanya vizuri kwa ajili ya kuchukua tena katika michezo ijayo,” alisema.

Related Posts