Dar es Salaam. Waswahili husema ‘mapenzi yanaua.’ Msemo huu unaweza kueleza tukio la Erick Buberwa kumuua mkewe bila kukusudia, baada ya kutokea ugomvi uliosababishwa na kunyimwa haki ya ndoa.
Hii ni baada ya Erick, wakiwa chumbani na mkewe Mercy Mukandala, kumuomba mkewe tendo la ndoa akakataa, akamwambia yeye (Mercy) ana mwanamume mwingine anayempenda zaidi yake hali iliyoibua ugomvi.
Kwa mujibu wa ushahidi uliopo katika rufaa ya Erick Buberwa iliyotolea Septemba 13, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, tukio hilo lilitokea usiku wa Juni 16, 2020, huko Tumbi mkoani Pwani.
Majaji watatu, Ferdnand Wambali, Lilian Mashaka na Benhaji Masoud, wameitupa rufaa ambayo Erick alikuwa akipinga adhabu ya kifungo cha miaka minane jela alichopewa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia.
Katika hukumu, majaji wamekataa hoja ya Jamhuri iliyotaka Mahakama hiyo itumie mamlaka yake na kubadili kifungo hicho cha miaka minane baada ya mahakama iliyosikiliza kuondoa miaka miwili aliyokaa mahabusu na kuwa kifungo cha miaka 20.
Majaji wamesema Jamhuri ilipaswa kuwasilisha rufaa kama iliona hairidhiki na adhabu aliyokuwa amepewa, lakini ikasema kwa vile hiyo haipo, basi mrufani atatumikia kifungo cha miaka minane alichohukumiwa Machi 17, 2022.
Ushahidi uliochambuliwa na jopo la majaji watatu, ni kuwa usiku wa Juni 16, 2020, Erick na Mercy waliokuwa mume na mke, walikuwa wamelala katika kitanda chao, Erick aliomba apewe haki yake ya ndoa.
Mercy alikataa, huku akimwambia ana mwanamume mwingine anayempenda zaidi kuliko yeye, kauli iliyosababisha ugomvi kati yao, hivyo Mercy alitoka chumbani na kwenda jikoni.
Ushahidi unaeleza alirejea akiwa amebeba bomba kwa lengo la kumpiga nalo mumewe ambaye alifanikiwa kumnyang’anya bomba hilo na kumpiga nalo kichwani.
Mercy aliangukia kwenye meza na kusababisha jeraha kubwa usoni. Jeraha hilo lilisababishwa atokwe damu nyingi hadi kupoteza fahamu.
Erick alimbeba na kwenda kumlaza kitandani kisha alitoka nje kwenda kuomba msaada kwa Herieth Dauson, aliyekuwa mfanyakazi wao wa ndani.
Herieth alipoingia chumbani, aliona matone ya damu kwenye meza na sakafuni, na hapo Erick akatoka nje kwenda kuwataarifu majirani waliofika chumbani na kumpeleka hospitali ya jirani walikoambiwa alikuwa ameshafariki dunia.
Mrufani alifikishwa kortini na kushitakiwa kwa kosa dogo la kuua bila kukusudia ambako alikiri na baada ya Mahakama kusikiliza maombolezo yake, ilimhukumu kifungo cha miaka minane jela baada ya kupunguza miaka miwili ya kukaa mahabusu.
Hata hivyo, hakuridhika na hukumu akakata rufaa akiegemea sababu mbili kubwa, kwamba Jaji alikosea kumpa adhabu kubwa bila kuzingatia alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na pia hakuzingatia maombolezo aliyoyatoa.
Sababu ya pili ni kuwa Jaji alikosea kisheria kwa kuonyesha upendeleo wakati wa kupima adhabu gani ampe na akazingatia tu kuwa kiini cha mauaji ni uchokozi uliotokana na mrufani kunyimwa haki yake ya tendo la ndoa.
Alieleza Jaji hakuzingatia vigezo vingine kama maneno ya uchokozi yaliyotolewa na Mercy kuwa ana mwanamume mwingine anayempenda zaidi na jaribio la mkewe la kutaka kumpiga kwa bomba.
Wakati rufaa ilipoitwa kusikilizwa Juni 12, 2024, wakili Mussa Mhagama alimwakilisha mrufani, wakati upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Job Mrema akisaidiana na John Mwakifuna.
Katika kujenga hoja zake, wakili Mhagama alisema mazingira ya namna kosa hilo lilivyotendeka hayakuzingatiwa na Jaji, kujielekeza vibaya katika dhamira ya kosa na hakuzingatia kuwa Erick anawajibika kumtunza mtoto wake wa kambo.
Mhagama alidai kumbukumbu za Mahakama zinaonyesha kulikuwa na kutokuelewana kati ya Mercy na Erick na kwamba, mrufani alikuwa amenyimwa haki yake ya tendo la ndoa.
Alidai Mercy ndiye aliyeleta bomba ndani ya chumba chao cha kulala ambalo baadaye lilitumika dhidi yake na si mrufani na kwamba, kunyimwa tendo la ndoa ndiyo iliamsha ugomvi baina yao.
Alidai Jaji aliyemhukumu kifungo cha miaka minane jela alipaswa azingatie kiini cha mauaji hayo kuwa ni maneno yaliyotamkwa na mke kwa mumewe. Alidai Jaji alishindwa kuzingatia kuwa Erick ana mtoto wa kambo anayemtegemea.
Akijibu hoja hizo, wakili Mrema alipinga rufaa hiyo akiegemea sababu mbili, moja ni kuwa Jaji aliyemhukumu Erick alitenda haki na pili akaomba Mahakama iongeze adhabu aliyokuwa amepewa kutoka miaka minane hadi miaka 20 jela.
Alisema ingawa ni kweli kuwa Mercy ndiye aliyekwenda chumbani na bomba hilo, lakini ushahidi ulio juu ya tukio hilo ni kuwa alipigwa na kutokana na kupigwa na bomba hilo, alipata majeraha mabaya kichwani.
Baada ya kusikiliza hoja za mawakili, majaji walisema Mahakama ya Rufani inaweza kuingilia adhabu aliyopewa mkosaji pale tu ambapo itabainika adhabu hiyo ni kinyume cha sheria.
Walisema kwa kawaida, mshitakiwa anayekiri kosa hupewa adhabu ndogo labda kuwe na mazingira mengine yanayosababisha apewe adhabu kubwa na kwamba, muda aliokaa mahabusu, unaweza kupunguzwa katika adhabu yake.
Majaji walisema hawaoni sababu ya kuingilia hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani na kwamba, kwa kuangalia ripoti ya daktari aliyeuchunguza mwili wa marehemu, alikuwa amepata majeraha mabaya yaliyomsababishia umauti.
“Tunakubaliana na hoja ya wakili Mhagama kuwa maneno ya marehemu ndiyo kiini cha ugomvi lakini tunajiuliza kutolewa kwa maneno hayo kunahalalisha kitendo alichokifanya mrufani?” inaeleza sehemu ya hukumu ya majaji.
“Je mrufani (Erick) alikuwa na uhalali wa kutumia nguvu kubwa kiasi kile kwa sababu tu amenyimwa tendo la ndoa? Tunakubaliana na Jaji kuwa kunyimwa tendo la ndoa siyo sababu ya kuweza kukatisha uhai wa mtu,” inaeleza.
Majaji hao wanasema Jaji aliyemhukumu mrufani alikuwa sahihi kuzingatia aina ya silaha iliyotumika kumpiga nayo marehemu na kwamba, mwongozo wa hukumu kwa makosa ya aina hiyo unatoa adhabu ya kati ya miaka 10 na kifungo cha maisha jela.
Katika hukumu, majaji wamekataa hoja ya Jamhuri iliyotaka mahakama itumie mamlaka yake na kubadili kifungo hicho cha miaka minane baada ya mahakama iliyosikiliza kuondoa miaka miwili aliyokaa mahabusu, na kuwa kifungo cha miaka 20.
Majaji wamesema Jamhuri ilipaswa kuwasilisha rufaa kama iliona hairidhiki na adhabu aliyokuwa amepewa lakini wakasema kwa vile hiyo haipo, basi mrufani atatumikia kifungo cha miaka minane alichohukumiwa Machi 17, 2022.