Dabi ya Dodoma ardhi ya ugenini

UMESHAWAHI kushuhudia mchezo wa dabi ukipigwa katika ardhi ya ugenini? Basi leo ndiyo itatokea hivyo pale Dimba la Tanzanite Kwaraa lililopo Manyara pindi Fountain Gate inayonolewa na kocha Mohamed Muya ikiikaribisha Dodoma Jiji ya Mecky Maxime.

Kama inavyofahamika mchezo wa dabi huwa baina ya timu zinazotokea eneo moja la mji, hivyo mchezo huu wa leo unazikutanisha timu zote zinazotokea Dodoma lakini kwa muda zimehamishia makazi Manyara.

Fountain Gate tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara iliuchagua Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa mechi za nyumbani, hivyo leo itakairibisha Dodoma Jiji ambayo nayo imehamia kwa muda uwanjani hapo kutokana na ule wa Jamhuri uliopo Dodoma kufungiwa.

Timu hizo kila moja msimu huu imefanya vizuri ndani ya uwanja huo ambapo zote zimeshinda mechi moja. Fountain Gate ilikuwa ya kwanza kushinda 2-1 dhidi ya KenGold mechi ikichezwa Septemba 11, kisha Septemba 12 Dodoma Jiji ikaichapa Namungo 1-0.

Katika ligi msimu huu, timu zote zimeshuka dimbani mara tatu, Fountain Gate imekusanya pointi sita baada ya kucheza mechi tatu ikishinda mbili dhidi ya Namungo (2-0) na KenGold (2-1), kisha ikapoteza moja dhidi ya Simba (4-0).

Dodoma Jiji ilianza ligi kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Mashujaa, kisha ikatoka 0-0 na Pamba, ikaifunga Namungo 1-0. Ina pointi nne.

Katika ligi, timu hizo msimu uliopita zilikutana mara mbili wakati Fountain Gate ikitumia jina la Singida Big Stars kisha baadaye ikaitwa Singida Fountain Gate.

Rekodi zinaonyesha kwamba, katika mechi zote mbili hizo, Dodoma Jiji ilipoteza nyumbani na ugenini. Mechi ya kwanza ilifungwa 2-1, kisha ikapata kipigo kingine cha mabao 2-0.

Msimu wa nyuma yake kwa maana ya 2022/23, kabla ya kuitwa Fountain Gate ilikuwa inaitwa Singida Big Stars, iliibuka kifua mbele dhidi ya Dodoma Jiji kwa kushinda mechi moja (1-0) na nyingine matokeo yakiwa 0-0.

Katika mchezo wa leo, Dodoma Jiji ina kazi kubwa ya kufanya kumaliza uteja wao mbele ya Fountain Gate, wakati wenyeji wakitaka kuendeleza ubabe wao.

Mohamed Muya ambaye ni kocha wa Fountain Gate, anaamini ushindi wa mechi mbili zilizopita unazidi kuwapa nguvu vijana wake katika kuendelea kufanya vizuri ikizingatiwa kwamba hawataki kupoteza nyumbani.

“Ni mchezo ambao tumejiandaa vizuri kushinda, sisi ni wenyeji na ushindi utazidi kutuweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo. Wapinzani wetu nao ni wazuri lakini nimewaandaa vijana wangu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo.

Agustino Nsata ambaye ni nahodha wa Dodoma Jiji, alisema; “Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri, tunafahamu mchezo hautakuwa rahisi kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji tunafahamiana, lakini mwalimu ameshafanya kazi yake na sisi tunakwenda kumalizia kilichobaki ndani ya uwanja.”

Related Posts