KenGold bado haijakata tamaa | Mwanaspoti

LICHA ya kudondosha pointi sita katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu Bara inayoicheza kwa mara ya kwanza, kocha mkuu wa KenGold, Fikiri Elias amesema bado ana imani ya timu hiyo kufanya vizuri kadri inavyozidi kuizoea ligi.

Wageni hao wa Ligi Kuu kutoka jijini Mbeya, kesho Jumatatu watavaana na KMC na kocha Elias alisema ana matumaini ya kuzindukia katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.

KenGold  ilianza msimu nyumbani kwa kufumuliwa mabao 3-1 na Singida Black Stars kisha kulala tena 2-1 mbele ya Fountain Gate ikiwa ugenini, lakini kocha Elias alisema vipigo hivyo vimewaamsha kwani wameshagundua udhaifu wa safu ya ulinzi na wameanza kuifanyia kazi mapema.

“Ukiangalia eneo la ushambuliaji linaonyesha kuna uhitaji wa kupambana na kupata nafasi za kufunga, walinzi mara nyingi ndio wamekuwa na makosa madogo madogo ambayo yanafundishika, tayari nimelifanyia kazi eneo hilo na wameniahidi kuwa hawatarudia makosa,” alisema Elias aliyetua klabuni hapo akitokea Coastal Union.

“Maeneo mengine yote yapo vizuri kwani timu ina uwezo wa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi lakini kulinda mabao ndio imekuwa shida. Kuelekea mchezo wetu wa Jumatatu ugenini tutakuwa na mwanga na ndio mchezo utakaoturudisha kwenye ushindani,” aliongeza kocha huyo.

Elius alisema katika mchezo wa kesho dhidi ya KMC ataingia kwa kumheshimu mpinzani ambaye amekiri kumfuatilia katika mechi zilizopita na kubainisha ameona ubora na upungufu wake, hivyo atatumia mbinu bora ili kuweza kupata matokeo ambayo yatamuweka kwenye nafasi nzuri ya kuisaidia timu hiyo kufikia malengo.

Kocha huyo alisema kwa ajili ya mchezo huo wameshaanza kusahihisha makosa waliyoyafanya katika mechi zilizopita ili kujiweka tayari na mchezo ujao ambao amekiri kuwa ni muhimu kwao kufufua matumaini.

KMC inarudi nyumbani baada ya awali kulazimishwa suluhu na Coastal Union kabla ya kwenda kucheza ugenini dhidi ya Singida BS na kulala 2-1 mjini Singida, huku kocha wa timu hiyo, Abdulhimid Moallin akisema haitakuwa rahisi kuangusha tena pointi ikiwa nyumbani kwani ameshajua kilichowaangusha awali.

Kocha huyo raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia, alisema licha ya safu ya ushambuliaji kufunga mabao mawili hadi sasa, lakini bado imekuwa ikipoteza nafasi nyingi wanazozitengeneza na sasa wanaenda kuweka mambo sawa dhidi ya KenGold.

Moallin aliyewahi kuinoa Azam, alisema licha ya ukuta wake kuruhusu mabao lakini washambuliaji wamekuwa na changamoto ya kutumia nafasi nyingi wanazotengeneza na kujikuta wanamaliza dakika 90 wakiwa wamepachika bao moja na kuruhusu wapinzani kuwatawala.

“Ukuta una shida yake lakini endapo washambuliaji wangekuwa wanafanya kazi yao kwa usahihi kwa kupachika idadi kubwa ya mabao tungekuwa tunazungumza mambo mengine, hapa kuna kazi natakiwa kuifanya ili kuibadili safu yangu ya ushambuliaji iwe tishio kama msimu ulioisha,” alisema.

Related Posts