Dar es Salaam. Ikiwa imepita miaka 15 tangu Mahakama ya Rufani ilipotengua uamuzi wa Mahakama Kuu uliotamka wagombea binafsi wana haki ya kushiriki uchaguzi nchini mwaka 2009, hoja hiyo imeibuka tena, wadau wakitaka haki hiyo irejeshwe kwenye mifumo ya uchaguzi.
Hoja hiyo imeibuliwa Septemba 14, 2024 na mwanasiasa na mwanataaluma, Profesa Anna Tibaijuka alipotoa mada kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jijini Dar es Salaam.
Profesa Tibaijuka amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kurejea suala hilo ili kuimarisha mfumo wa demokrasia.
Kwa muda mrefu aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha DP, marehemu Christopher Mtikila alipigania haki hiyo kwa hatua mbalimbali na hata alipopewa ushindi na Mahakama Kuu, baadaye uliteunguliwa na Mahakama ya Rufani, iliyohitimisha kuwa “suala hilo ni la kisiasa ambalo linaweza kumalizwa na Bunge”.
Mchungaji Mtikila hakukata tamaa, alienda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), ambayo Julai 2013 ilikubaliana na hoja zake Mtikila aliyefungua kesi pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Katika hukumu AfCHPR ilikubali kuwa Tanzania ilikiuka haki za raia kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi yao moja kwa moja au kupitia wawakilishi kwa kulazimisha raia kuwa wanachama wa vyama vya siasa ili wapate kibali cha kugombea urais, ubunge na serikali za mitaa.
Ilielekeza Serikali ifanye marekebisho ya sheria ili kuruhusu haki hiyo.
Kauli ya Profesa Tibaijuka
Akitoa mada katika maadhimisho hayo, Profesa Tibaijuka aliyewahi kuwa mbunge na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesema licha ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, imejikita kwenye “udikteta wa vyama”.
“Kwa nchi hii kuna tatizo. Katiba yetu inasema kama unataka kugombea ni lazima ujiunge na chama na hilo ni kwa kila mtu, kwa hiyo hapa tuna demokrasia ya vyama lakini ni udikteta wa vyama. Ni kwa nini mgombea huru asiruhusiwe?” amehoji.
Profesa Tibaijuka aliyekuwa anatoa mada kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa, amesema hicho ni kikwazo kwa kundi hilo.
“Hili ni tatizo ambalo Rais Samia kama ataweza afanye marekebisho ili aruhusu wagombea huru. Itasaidia wanawake, wanaume na Watanzania kuboresha uongozi wa siasa,” amesema.
Amesema hofu iliyopo miongoni mwa vyama vya siasa ni kusambaratika, endapo mgombea binafsi ataruhusiwa, jambo alilosema si sahihi.
“Mbona Marekani (vyama) havijapotea? Unaweza ukawa Democratic au Republican na unaweza kuwa huru. Hivyo ndivyo unaweza kuimarisha vyama.
“Hapa unyanyasaji wa viongozi watarajiwa unatokana na kunyimwa uhuru wa kugombea kama binafsi. Unajua wananchi wanapopiga kura hawapigii chama, wanampigia mtu,” amesema na kuongeza:
“Kwa hiyo vyama vimewafunga watu wenye mawazo tofauti, kwamba wakae kweye msimamo wa chama.”
Amesema mfumo wa vyama vya Tanzania umeiga ule wa Kisovieti wa Russia, ukiwa na muundo wa vikao kwa ngazi za mkutano mkuu, halmashauri kuu na kamati kuu.
Hoja ya Profesa tibaijuka imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo aliyeshiriki katika jopo la majadiliano akisema huo pia ni msimamo wa chama hicho.
“Naungana na Profesa Tibaijuka, kwa nini tusiwe na mgombea huru? Huo ndiyo msimamo wa UDP. Huko kwenye vyama usiponunua madera, unawekwa nje, usipokuwa na hela au maokoto huna nafasi.
“Tumefika mahali Tanzania, uchaguzi umekuwa mnada, hakuna hela hakuna uongozi, kama una hela watupie uwe mbunge, kama huna hela kaa nyumbani,” amesema.
Akieleza mwenendo wa demokrasia nchini, Profesa Tibaijuka aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), amesema demokrasia inapiganiwa na hata mfumo wa vyama vingi nchini ulipiganiwa na Mwalimu Julius Nyerere.
“Tanzania imeingia kwenye demokrasia ya vyama vingi, haikuwa hivihivi, bali mapambano, na aliyepambana ni Mwalimu Julius Nyerere,” amesema.
Amewataka vijana kupigania demokrasia na haki za kijinsia.
“Kwa ninyi vijana, hakuna kitu kitakuja bure kwenye sahani, ni lazima tupambane. Mimi nilianzisha Baraza la Wanawake Tanzania likafutwa na Serikali, lakini sikukata tamaa, kwa sababu nilikuwa najua wakati wake haujafika,” amesema.
Akichangia suala hilo, Askofu Emmaus Mwamakula wa la Moravian Revival Church amesema kuna janga la vyuo vikuu kushindwa kuandaa vijana wanaopambania demokrasia, badala yake wanakuwa ‘chawa’.
“Zamani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilikuwa kinandaa vijana na kiuongozi. Vijana walikuwa ni sehemu ya kukuza vipaji, lakini sasa vyuo vikuu vimekua ni sehemu ya kuunda machawa wa vyama na watawala.
“Hakuna mijadala tena kwenye vyuo vikuu na hali imekuwa mbaya na hata wahadhiri kwenye vyuo vikuu wamekuwa machawa. Sasa kwa hali kama hii nchi yetu inakuwa mbaya sana,” amesema akimaanisha wasomi hao wanajikomba kwa viongozi kwa masilahi binafsi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Rehema Sombi amesema Rais Samia ameleta falsafa ya 4R inayolenga kuboresha demokrasia.
“Tuko kwenye awamu ya sita ya Rais Samia , amekuja na falsafa ya maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu na kujenga upya, hiyo ni misingi imara ya kufanya demokrasia ijengwe upya,” amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu amesema mapambano ya kidemokrasia kwa wapinzani ni magumu, ikiwa ni pamoja na kupoteza makada wao na wengine kuuawa.
“Mimi nauliza, for how long shall they kill our prophets? (Hadi lini wataendelea kuua manabii wetu),” amehoji Pambalu akinukuu mashairi ya wimbo wa Bob Marley uitwao Redemption Song.
Pambalu amerejea tukio la kutekwa na kuuawa kwa kada wa chama hicho, Ali Mohamed Kibao na kupotea kwa makada wa chama hicho, akihoji, “mpaka lini?”
Ushiriki wa wanawake, vijana, wenye ulemavu
Akieleza ushiriki wa wanawake katika siasa, Profesa Tibaijuka amesema kumekuwa na ongezeko wa kundi hilo kwenye vyombo vya uamuzi.
“Kumekuwa na maendeleo bungeni, kutoka asilimia 3.4 katika uchaguzi wa mwaka 1995 ya wanawake katika majimbo hadi asilimia 10.4 katika uchaguzi wa mwaka 2020,” amesema.
Profesa Tibaijuka amepongeza mfumo wa vyama vya upinzani katika kuwaandaa wagombea wanawake.
“Nadiriki kusema, wanawake wa vyama vya upinzani wanafanya vizuri kuliko wanawake wa CCM. Mimi ni mwanamke wa CCM na huo ndiyo ukweli kwa sababu wana mpangilio mzuri.
“Ukiangalia Chadema, huwezi kugombea viti maalumu kama hujajaribu kwenye jimbo. Lakini CCM ni kinyume, ukienda jimboni unajifungia kwenye viti maalumu,” amesema.
Akieleza uzoefu wake katika uchaguzi, Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amesema kuna changamoto ya mwanamke kugombea uongozi na hasa akiwa vyama vya upinzani.
“Kwa mfano wakati wa uchaguzi, kwenda tu kuchukua fomu ni vita, inabidi utafute vijana. Mimi siku narudisha fomu ya chama, nilipigwa mabomu, lakini sheria zipo na hazitekelezwi,” amesema.
Ameeleza jinsi alivyokabiliana na polisi baada ya kudai mabadiliko ya ratiba ya kampeni katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 katika jimbo la Serengeti mkoani Mara.
“Nilipigwa na askari 12 na nilitolewa pale nikiwa sina blauzi nikapelekwa kituo cha polisi. Kwa mambo haya nani atakubali kushiriki siasa?” amehoji.
Ushuhuda kama huo ulitolewa na Katibu wa Idara ya Uchaguzi na Mipago wa Ngome ya Wanawake wa chama cha ACT-Wazalendo, Mary Mongi aliyegombea udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Kwanza ukiwa mwanamke, familia yenyewe inakuona umeamua kuacha mume, watoto kwa ajili ya kupambania mambo ambayo yanaweza kukutoa uhai,” amesema.
Akizungumzia nafasi ya vijana katika ushiriki wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Bridge for Change, Ocheki Msuva amesema kundi hilo halipewi nafasi ya kutosha kwenye ngazi za uamuzi.
“Changamoto kwenye mfumo wa vyama vya siasa, kuna tawi la vijana, ukiwauliza ni kama vile wako kwenye chumba cha matarajio ya uongozi,” amesema.
Ametaja changamoto za kisheria, akiitaja Sheria ya Makosa ya Mitandao kuwa inakwaza katika utoaji wa maoni kwa vijana.
“Changamoto ya pili ni elimu ya uraia na uelewa wa masuala ya uchaguzi na michakato ya kidemokrasia. Kwanza utoe taarifa hapa, upate kibali, hivyo vyote vinazuia elimu,” amesema.
Akizungumzia changamoto za watu wenye ulemavu, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki za Kiraia Kiuchumi kwa Watu wenye Ulemavu, Gideon Mandes amesema licha ya Katiba kuwapa haki ya kushiriki siasa, wanakwama.
“Changamoto kubwa kwanza elimu ya uraia na wapiga kura, idadi kubwa ya wenye ulemavu hawana elimu hivyo, pili ni ugumu wa mawasiliano na upatikanaji wa taarifa muhimu,” amesema.
Ametaja pia changamoto ya umasikini akisema inawadhoofisha kushiriki siasa.
“Pia kuna ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu. Mara nyingi vyama vya siasa wanaangalia ulemavu bila kuangalia uwezo wa mtu. Ulemavu siyo kushindwa,” amesema.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.