Sababu Udart kusitisha ‘mwendokasi’ Kibaha

Dar es Salaam. Uhaba wa mabasi unatajwa na Kampuni ya Uendeshaji Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), kuwa sababu za kusitisha huduma ya usafiri huo kwenda Kibaha, mkoani Pwani.

Mradi wa mabasi hayo ulianza kufanya kazi rasmi Mei 2016 katika Barabara ya Morogoro ukiwa na mabasi 210, huku mahitaji yakiwa ni mabasi 305.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 14, 2024, msemaji wa kampuni hiyo, Katanga Gabriel, amesema huduma ya mabasi kwenda Kibaha ilisitishwa wiki moja iliyopita.

Amesema uchache wa mabasi ni sababu ya kusitisha safari akieleza mahitaji ya mabasi ni makubwa kuwezesha kutoa huduma kwa miundombinu iliyopo.

“Mmekuwa mkisikia mara kwa mara kuwa tumekuwa na mabasi machache huku abiria wanaohitaji huduma wakiwa ni wengi, hivyo tumeona safari za kwenda Kibaha tuzisitishe kwanza mpaka hapo mabasi mengine yatakapoongezwa,” amesema Gabriel.

Alipoulizwa ni lini hasa huduma hiyo itarejeshwa, amesema ni mpaka hapo mabasi 100 ambayo Serikali inatarajia kuyaagiza yatakapoletwa.

Julai 15, 2024, akizungumza  na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema Serikali inatarajia kuongeza mabasi 100 ya mwendokasi ili kutatua changamoto ya usafiri huo.

Katika mkutano huo, Mchechu alisema mabasi hayo yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB.

“Kwa kipindi cha miezi miwili nimekuwa nikifanya vikao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), Kampuni ya Mabasi Yendayo Haraka (Udart), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).

“Nafikiri kwa sasa tumefikia ukingoni maana tumeona inaenda kuleta crisis (mgogoro) na kuathiri taswira nzuri ya Serikali,” alikaririwa alisema Mchechu.

Kwa mujibu wa Mchechu mabasi hayo yatakuwa yamewasili nchini ndani ya miezi sita ijayo ili kusaidia kutatua changamoto ya usafiri huo.

Mbali na Mchechu, Agosti 2, 2024, alipozindua mageti na kadi janja kwa ajili ya usafiri wa mabasi hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa aliagiza hadi ifikapo Desemba 2024, mabasi yanayotakiwa katika barabara ya Morogoro na ile ya Mbagala yawe yamepatikana.

Katika maagizo hayo, alizitaka mamlaka zinazosimamia usafiri huo (yaani Dart na Udart) kuacha danadana katika kufanikisha hilo kwa kuwa wananchi wamechoshwa na ahadi hewa.

Katika kufanikisha hilo, Mchengerwa alisema hakuna haja ya kuwasubiri wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa kuwa wapo Watanzania wengi wanaweza na kutaka wapewe nafasi wakiwemo wamiliki wa mabasi ya mikoani.

“Taarifa nilizonazo ni kwamba barabara ya Morogoro inahitaji mabasi 170, huku ile ya Mbagala ikihitaji mabasi 500, hivyo nataka yapatikane kabla ya Desemba, mwaka huu nina hakika tuna Watanzania wanaliweza hilo washirikisheni wakiwemo wamiliki wa mabasi,” alisema.

Mmoja wa wakazi wa Kibaha waliokuwa wakitumia usafiri huo, James Liamba amesema tangu awali Serikali ilikurupuka kuweka usafiri huo kwenda Kibaha huku ikijua ina mabasi machache.

Jamila Kibwana, mkazi wa Mbezi amesema pamoja na kusitishwa huduma ya kwenda Kibaha, bado hawajaona ahueni ya kupatikana kwa usafiri huo akisisitiza dawa ni kuongezwa kwa mabasi.

Related Posts