BAO moja lililofungwa na Prince Dube dakika 45 kipindi cha kwanza dhidi ya CBE SA ya Ethiopia limetosha kuitanguliza Yanga mguu mmoja mbele katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikivunja mwiko wa kutiopata ushindi katika ardhi ya nchi hiyo katika michuano ya CAF.
Ikicheza kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa, Yanga itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi mnono kutokana na kutengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia katika vipindi vyote vya mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa.
Dube, aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Azam FC, licha ya kutumia nafasi moja ya dhahabu kwa timu yake alishindwa kushangilia bao hilo badala yake aliomba radhi kwa benchi la ufundi kutokana na kushindwa kutumia nafasi nyingi alizozipata.
Nyota huyo wa kimataifa aliyeanzishwa sambamba na Stephane Aziz KI, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, huku eneo la kiungo likiwa chini ya Khalid Aucho na Mudathir Yahya alifunga bao hilo akipokea pasi kutoka kwa Aziz na kumchengesha kipa wa CBE kabla ya kufungwa eneo la juu.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kuhitaji sare yoyote katika mechi ya marudiano wikiendi ijayo itkayopigwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar ili kuandika historia ya kucheza makundi kwa msimu wa pili mfululizo baada ya msimu uliopita ikiwa ni baada ya kupita miaka 25 tangu ilipocheza kwa mara ya kwanza 1998.
Ushindi huo ni muendelezo wa rekodi kwa Kocha Miguel Gamondi ambaye ndiye aliyeipeleka Yanga makundi baada ya miaka 25 na kuishia robo fainali, baada ya awali kuvunja mwiko wa Al Merrikh ya Sudan waliyoifunga raundi ya pili kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda ugenini 2-0 na nyumbani 1-0.
Rekodi zinaonyesha Yanga haijawahi kuifunga timu kutoka Ethiopia ikicheza nyumbani kwao, kwani mechi nne zilizopita ilitoka sare mbili na kupoteza mbili ikiwamo mara ya mwisho mwaka 2018 ilipolala 1-0 kwa Welayta Dicha katika Kombe la Shirikisho, lakini ushindi wa nyumbani wa 2-0 ukaivusha kuingia makundi.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza kwa kasi kabla ya wenyeji wao ambao wanacheza soka la kutembeza boli chini kujibu mapigo lakini uimara wa kipa Djigui Diarra na mabeki wa timu hiyo ukafanya mchezo kuendelea kuwa mgumu kwa pande zote hadi sekundu chache kabla ya mapumziko Dube alipofunga bao hilo baada ya kosa kosa nyingi.
Katika kipindi cha pili Yanga iliendeleza moto na kupoteza nafasi za wazi, kabla ya kocha Gamondi kufanya mabadiliko dakika ya 65 kwa kuwatoa kwa mpigo, Dube na Aziz Ki na kuwaingiza Clement Mzize na Clatous Chama ambao nao walipoteza pia nafasi kadhaa kwa kukosa umakini.
Gamondi alifanya mabadiliko kwa kumtoa Maxi ili kumpisha Yao Kouassi, huku Pacome na Mudathir Yahya nao wakitolea kuwapisha Jean Baleke na Duke Abuya. Baleke huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa kimataifa akiwa na Yanga, kwani mechi mbili za raundi ya kwanza dhidi ya Vital’O ya Burundi hakucheza kwa ishu za vibali, lakini hata hivyo bado hakukuwa na maajabu kwa wageni hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi, Issa SY kutoka Senegal ilipolia kuashiria kumalizika kwa pambano hilo.
Kikosi cha Yanga kinajiandaa kurejea nchini ili kujiandaa na mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumamosi ijayo na mshindi wa jumla atafuzu makundi.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo, Al Merrikh ya Sudan imelazimishwa sare ya 2-2 na FA Rabat ya Morocco, huku TP Mazembe ikicheza ugenini imeikandika Red Arrows kwa mabao 2-0, wakati katika Kombe la Shirikisho Zamalek imeichapa Polisi Kenya kwa bao 1-0 jijini Nairobi.