Tabora Utd, yabanwa nyumbani | Mwanaspoti

WENYEJI Tabira United imeshindwa kuendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu Bara baada ya jioni hii kulazimishwa suluhu na Tanzania Prisons ambayo haijaonja kabisa ushindi msimu huu.

Tabora iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita kupitia mechi za play-off dhidi ya Biashara United ya Ligi ya Championship, ilianza msimu kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba kabla ya kuzinduka na kushinda michezo miwili mfululizo iliyoafuata mbele ya Namungo na Kagera Sugar.

Hata hivyo, katika mechi ya leo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora, Nyuki hao walijikuita wakishindwa kufurukuta mbele ya maafande hao ambao hiyo ni suluhu la tatu mfululizo tangu msimu uanze baada ya awali kutoka 0-0 na Pamba Jiji kisha Mashujaa na kuifanya ifikishe pointi tatu.

Wenyeji walipewa nafasi kubwa na mashabiki kutoka na ushindi nyumbani, kutokana na Prisons kucheza kwa akili na kuzuia nyavu zao zisiendelee kuguswa hadi sasa, licha ya wachezaji Yacouba Songne kupata nafasi kadhaa na kuzipoteza.

Wakati mchezo ukiendelea  vita kubwa ilikuwa kati ya beki beki wa kati wa Tabora, Kelvin Pemba dhidi ya mshambuliaji wa Prisons, Samson Mbangula jambo ambalo liligeuka kivutio kwa mashabiki waliojitokeza katika mchezo huo kumshangilia beki huyo ambaye tangu kuanza kwa ligi amekuwa na kiwango bora ambapo pamoja na mambo mengine beki huyo ndiye ameibuka mchezaji bora wa mchezo huo.

Baada ya mchezo kumalizika, kocha wa Prisons Mbwana Makatta amesema wachezaji wa timu hiyo kutopata matokeo katika mchezo huo kumetokana na kutotumia nafasi walizopata.

“Nawapongeza wachezaji wetu wamecheza kwa kiwango kikubwa, shabaha yetu ilikua ni kumaliza mchezo mapema lakini  mpaka mwisho tumepata sare ya bila kufungana jambo ambalo ni faida kubwa kwa upande wetu maana tumeanzia ligi ugenini kwa michezo mitatu na hatujaruhusu kufungwa hadi sasa,” amesema Makatta na kuongeza;

“Kipindi cha kwanza tulicheza kwa kupokezana na wapinzani wetu waliokuwa bora, lakini kipindi cha pili niliongeza wachezaji wenye kasi kubwa waliotufanya tucheze kwa muda mrefu na tulitengeneza baadhi ya nafasi tulizoshindwa kuzitumia, hata hivyo makosa yalioonekana leo tutayafanyia kazi ili mchezo ujao tushinde.”

Kwa upande wa kocha wa Tabira, Francis Kimanzi amesema kitendo cha kucheza mechi ndani ya saa 72 kimechangia timu yake kutopata matokeo pamoja na kwamba hajutii sare aliyoipata kwenye mchezo huo.

“Wachezaji wamejitima na kitendo ccha kupata alama moja mbele ya Prisons haikuwa kazi rahisi kutokana na aina ya mpinzani tuliyekutana naye, tunashukuru kwa kuvuna alama tatu nyumbani si haba,” amesema kocha huyo raia wa Kenya na kuongeza;

“Hatukupata kabisa nafasi ya kupumzika baada ya mchezo wetu jumatano iliyopita lakini tulijiandaa hivyo hivyo na leo hatujapoteza, pamoja na hayo kuna nafasi kadhaa tumetengeneza ila hatujazitumia vizuri ila ndio soka tutajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya Fountain gate ili tupate matokeo.”

Mchezaji Salum Chuku ambaye amekuwa nguzo muhimu kwa Tabora katika mchezo wa leo, alishindwa kumaliza dakika 90 baada ya kupata majeraha na kuwahishwa hospitalini kwa gari la kubebea wagonjwa na kwa mujibu wa kocha Kimanzi, alikuwa akiendelea na matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete ambapo hali ilitengemaa ataruhusiwa kujiunga na wenzake.

Kwa matokeo hayo Tabora imepanda hadi nafasi ya tatu ikifikisha pointi saba kama ilizonazo Mashujaa ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, zikiwa nyuma ya vinara Singida Black Stars yenye pointi tisa baada ya mechi tatu., huku Prisons ikifikisha alama tatu kupitia michezo mitatu pia.

Related Posts