Songwe. Wadau wa afya nchini wameeleza mchango wa Dk Daimond Simbeye aliyekuwa mtaalamu wa afya ya umma hasa tohara ya matibabu ya kiume ya hiari (VMVC), inayochangia kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60.
Dk Simbeye (56) aliyezikwa katika Kijiji cha Mbulu wilayani Mbozi, alifariki Septemba 9, 2024 baada ya kuugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Mloganzila Dar es Salaam.
Akizungumza katika mazishi yaliyofanyika Septemba 13, 2024, Mkurugenzi wa Miradi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Tanzania (CDC) kutoka Ubalozi wa Marekani, George Mgomella amesema kifo cha Dk Simbeye ni pigo kwa Taifa kutokana na mchango alioutoa katika udhibiti wa maambukizi ya VVU.
Dk Mgomela amesema Dk Simbeye ameitumikia CDC kwa miaka 12, ambapo alishiriki katika udhibiti wa maambukizi hayo akiendesha kampeni ya tohara ya matibabu ya kiume ya hiari (VMMC).
“Uongozi wake na utaalamu wake ulikuwa muhimu katika kusaidia jitihada za VMMC za Tanzania kufikia malengo na kuzidi malengo kwa wakati pia kuboresha ubora wa huduma katika mazingira ya jamii,” amesema Dk Mgomela.
Amesema katika kampeni hiyo, vijana wanaofikia miaka 15 wapatao 800,000 hadi 900,000 walifikiwa na huduma hiyo kila mwaka.
“Simbeye alikuwa anaangalia fedha kutoka mfuko wa Rais wa Marekani (PEPFAR) ili kusaidia kundi hilo la vijana kuwezeshwa kufanyiwa tohara bure nchini Tanzania,” amesema Dkt Mgomela.
Mratibu wa tohara kutoka Wizara ya Afya, Susan Mmbando amesema marehemu katika kampeni hiyo, alifanikisha wanaume zaidi ya milioni sita kufanyiwa tohara katika mikoa 17 nchini.
Amesema amemfahamu Dk Simbeye kwa miaka 25 akiwa mtumishi wa umma na baadaye mtumishi wa CDC.
“Nimefanya naye kazi akiwa CDC katika masuala ya tohara kwa wanaume, hivyo mchango wake kwa Serikali ni kusimamia mikoa saba ya mfano katika tohara ambayo ni Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara, Kigoma na Kagera ikiwa ni miongoni mwa mikoa 17 ya kipaumbele.
“Kwa mara mwisho tulikuwa na marehemu Dk Simbeye mkoani Morogoro kuanzia Septemba 2 hadi 6, 2024 tukitengeneza mpango endelevu wa tohara na alikuwa na michango mingi ya muongozo huo,” amesema Mmbando.
Dk Simbeye alizaliwa Juni 28, 1968 katika kijiji cha Msia kata ya Chitete wilayani Ileje Mkoani Songwe na kufariki Septemba 9, 2024 akiwa na miaka 56.
Ameacha mke mmoja na watoto watatu kati yao wa kiume wawili na mmoja wa kike.