Maofisa uandikishaji na mawakala wa vyama vya siasa Manyara watakiwa kushirikiana

Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji Mkoa wa Manyara kutumia elimu na ujuzi walioupata kwenye mafunzo ya uandikishaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza katika mafunzo kwa watendaji hao Jaji wa Mahakama kuu Tanzania, Asina Omar amesema watendaji hao wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na moyo wa kujituma pamoja na kutumia uzoefu walionao ikiwemo Elimu waliyoipata ili kukamilisha zoezi hilo.

“Matarajio ya tume Kutokana na mafunzo haya kila mmoja wenu atapata elimu na ujuzi wa kutosha utakaowezesha kutekeleza majukumu yake ili kufanikisha uboreshaji wa daftari,mafunzo haya yatahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kujiandikisha wapiga kura”.

Aidha,amesema wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kusaidia kuleta uwazi katika zoezi Zima.

“Lakini pia mawakala hao watasaidia kuwaambua waombaji wa maeneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima” alisema Asina

Aidha msisitizo wa tume ni uleule kwa mawakala wa vyama vya siasa kwamba hawatoruhusiwa kuingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la Kudumu la wapiga kura vituoni.

Maafisa uchaguzi wasaidizi wilaya za Kiteto na Mbulu mjini wamesema wamejipanga kuwahudumia Wananchi wote na kwamba wanaendelea na uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na matangazo ya gari mtaani.

  

Related Posts