Sudan Kusini yaahirisha uchaguzi wake Desemba, sasa kufanyika 2026

Juba. Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuusogeza mbele uchaguzi wake mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 2024, hadi Desemba 2026 huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni kutofanyika kwa maandalizi. 

Awali, uchaguzi huo ulipaswa kufanyika Desemba 22, 2024, lakini umeahirishwa tena ikiwa ni mara ya pili kuahirishwa. Hata hivyo, Ofisi ya Rais Salva Kiir imesema kuna changamoto zinazoukabili mchakato wa amani nchini humo.

“Ofisi ya Rais, chini ya uenyekiti wa Rais Kiir, imetangaza kuongeza muda wa mpito kwa miaka miwili pamoja na kuahirisha uchaguzi ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 2024 hadi Desemba 22, 2026,” imesema Ofisi ya Kiir kwenye ukurasa wake wa Facebook kama ilivyonukuliwa na shirika la habari la Al Jazeera.

Hata hivyo, Serikali imesema inahitaji muda zaidi kukamilisha michakato kama vile sensa, uandishi wa Katiba ya kudumu na usajili wa vyama vya kisiasa kabla ya uchaguzi kufanyika, kwa mujibu wa mshauri wa Rais kuhusu usalama wa kitaifa, Tut Gatluak.

“Unahitajika muda wa ziada kukamilisha kazi muhimu kabla ya uchaguzi,” imesema Ofisi ya Rais Kiir.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi ambao umesababisha watumishi wa umma kukosa mshahara kwa karibu mwaka mzima.

Hiyo ni baada ya mauzo yake ya mafuta kuathirika kutokana na bomba linalosafirisha mafuta hayo kuharibiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe  .

Hivyo, baraza la mawaziri limeidhinisha jana Jumamosi kuongezwa kwa muda wa miaka miwili wa kipindi cha mpito kilichokubaliwa na pande zilizokuwa na mzozo mwaka 2018, pamoja na kuahirisha uchaguzi mkuu wa kwanza kwa kipindi hicho tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Sudan, mwaka 2011.

Rais Kiir na mpinzani wake wa zamani aliyegeuka kuwa makamu wa Rais, Riek Machar, walitia saini makubaliano ya amani mwaka 2018 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano vikisababisha vifo vya takriban watu 400,000, njaa na ongezeko kubwa la wakimbizi.   

“Kulikuwa na baadhi ya vifungu katika mkataba wa amani ulioimarishwa ambavyo havikutekelezwa na hatutaki kuharakisha uchaguzi bila kutekeleza vifungu vyote,” amesema Waziri wa Mawasiliano na Huduma za Posta, Jacob Korok, baada ya mkutano wa baraza la mawaziri mjini Juba.

Rais Kiir na vyama vya siasa wamekubaliana kuahirisha uchaguzi ili kuruhusu matumizi ya miezi mitano iliyobaki ya mkataba wa amani ulioimarishwa na kipindi chake ambacho kinamalizika Februari 22, 2025, kwa ajili ya kutafuta fedha.

Makubaliano ya amani ya mwaka 2018 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe yaliruhusu Rais Salva Kiir kubaki madarakani katika serikali ya mpito huku mpinzani wake wa zamani, Machar akihudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais.

Related Posts