9 Bara bado hakijaeleweka | Mwanaspoti

WAKATI Ligi Kuu ikichezwa mechi tatu kwa baadhi ya timu, hali imeonekana kuwa tete kwa miamba tisa kutoonja ladha ya ushindi wala bao na nyingine zikiambulia vichapo.

Singida Black Stars iliyocheza mechi tatu hadi sasa ndio wameonekana kuwa imara wakishinda zote na kuongoza msimamo kwa pointi tisa na wastani mzuri wa mabao (manne) ya kufunga wakiruhusu bao moja.

Mashujaa waliomaliza msimu uliopita kwa kusuasua kupambana kushuka daraja, wameonyesha ubabe wakiwa nafasi ya pili kwa pointi saba, huku ndugu zao kikanda, Tabora United waliocheza mchujo wa kushuka daraja msimu uliopita wakiwa na alama saba baada ya michezo minne.

Timu ambazo mambo yamekuwa si shwari ni Kagera Sugar iliyocheza mechi tatu wakipoteza zote, wakifungwa mabao manne na kuwa mkiani wakiwa hawajaonja sare,  ushindi wala kupata bao la kuotea.

Matokeo kama hayo, yameikumba pia Namungo walioruhusu idadi kama hiyo ya mabao bila kufunga bao lolote na kuwa nafasi mbili za mkiani katika ligi hiyo.

Ken Gold wanaoshiriki ligi hiyo kwa msimu wa kwanza, hali imekuwa tete wakicheza mechi mbili wakiambulia vipigo, wakiruhusu wavu wao kuguswa mara tano huku wakifunga mabao mawili.

Coastal Union na KMC zilizocheza mechi mbili, zimeambulia pointi moja sawa na JKT Tazania waliocheza mchezo mmoja, huku Azam wakiambulia suluhu kwenye michezo miwili iliyocheza.

Pamba Jiji na Tanzania Prisons zimeendelea kupitia wakati mgumu kwa kushindwa kuonja ushindi katika michezo mitatu, zikipata sare mfululizo na kuvuna ponti tatu.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata alisema bado nyota wake wanakosa umakini katika umaliziaji wa mipira ya mwisho, huku akiwapongeza kwa kuvuna pointi tatu za ugenini.

“Tumeanzia ugenini michezo mitatu, hatujafungwa wala kufunga bao, si matokeo mabaya, lakini tulikosa umakini katika kumalizia nafasi tulizopata. Niahidi michezo inayofuata tutafanya vizuri,” alisema Makata.

Kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda alisema baada ya msukosuko waliopitia wa kukosa ushindi, kwa sasa mazungumzo yao kambini ni namna ya kujisahihisha ili mechi ya leo Jumatatu dhidi ya JKT Tanzania washinde.

“Stori kubwa kwetu kwa sasa ni namna tutakavyoondokana na matokeo haya, tunacheza vizuri ila ushindi ndiyo shida, tutajipanga kuona mechi inayofuata nyumbani tubadili upepo,” alisema kipa huyo.

Related Posts