Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kwa ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua, utafiti umeonyesha wengi wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo unyanyapaa.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Hakielimu katika wilaya 12 za mikoa sita nchini iliyotolewa Aprili 29, 2024 inaonyesha kwa kiasi kikubwa unyanyapaa unafanywa na walimu wakuu wa baadhi ya shule, huku kukiwa na vitendo vya udhalilishaji wa mabinti wanaojaribu kurejea shuleni.
Katika utafiti huo, asilimia 61.2 ya wahojiwa walieleza wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya udhalilishaji wanaokutana nao wakiitwa majina yasiyofaa na yanayokatisha tamaa.
Asilimia 53.2 walieleza licha ya shauku waliyonayo ya kurejea shuleni lakini wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutolewa mfano mbaya kila wakati.
Walimu wakuu pia wametajwa katika utafiti huo kuchangia mabinti waliopata ujauzito wasirejee shuleni kwa kile kilichoelezwa wanawakataa kwa hofu ya kuwaharibu wanafunzi wengine.
Kutokana na hali hiyo, wito umetolewa kwa Serikali kuweka mkazo kwenye utekelezaji wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.
Mwongozo huo ulitolewa Februari 2022, ulilenga kuwezesha urejeshwaji wa wanafunzi waliokatiza masomo katika shule za msingi na sekondari, kushirikisha wadau kuhusu wajibu wao katika kuwarejesha wanafunzi waliokatiza masomo baada ya Serikali kuruhusu kurejea shuleni.
Mtafiti Dk Joyce Mbepera amesema utafiti huo ulibaini wapo wakuu wa shule ambao wanakataa kuwapokea wanafunzi waliojifungua, licha ya mwongozo kuwapa jukumu la kuhamasisha wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.
Dk Joyce amesema utafiti huo ulibaini walimu wengi wakiwemo wakuu wa shule hawana uelewa wa kutosha kuhusu mwongozo huo.
“Asilimia 29.4 ya wahojiwa walieleza wamejaribu kurejea shuleni lakini wanakataliwa na wakuu wa shule wakihofia kuwafundisha wanafunzi wengine tabia mbaya. Tuna mfano wa mzazi ambaye alienda mara kadhaa shuleni kuomba mtoto wake arejee masomoni baada ya kujifungua lakini amekataliwa hadi sasa yupo nyumbani,” amesema.
Akizungumza pasipo kutaja jina lake, mama wa mtoto aliyefikwa na kadhia hiyo amesema: “Niko tayari kulea mjukuu na mtoto wangu anataka kurudi shule lakini mwalimu mkuu hataki kumpokea, sina uwezo wa kumhamishia kwingine naumia nikiona ndoto zake zinayeyuka.”
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebecca Gyumi amesema ipo haja kwa Serikali kuhakikisha kuna takwimu za uhakika na halisi za wasichana wanaorejea shuleni baada ya kujifungua.
Rebecca amesema kinachoonekana katika maeneo mengi mabinti wanakutana na mazingira magumu yanayowafanya waamue kukatisha tena masomo.
“Serikali imetoa mwongozo lakini kuna changamoto kubwa kwenye utekelezaji wa mwongozo huu, na mahali pengine wanaotakiwa kutekeleza hawajui majukumu yao au wanafanya ndivyo sivyo,” amesema.
Amesema, “nakubaliana na hicho kilichoelezwa kwenye ripoti kuhusu wakuu wa shule kwa kuwa kinachoonekana walimu wengi wanahangaika kuwasaidia mabinti wenye uwezo darasani, yaani kuna ubaguzi wanaoonekana kuwa wazito hawasaidiwi,” amesema Rebecca.
Ameshauri elimu ya afya ya uzazi kuwekewa mkazo kwa vijana wa rika balehe ili kuwaepusha na mimba za utotoni kwa kile alichoeleza, kama hawana elimu hiyo suala la mimba litaendelea kuwa tatizo sugu.
Mtafiti mshauri wa Hakielimu, Dk Wilbeforce Meena amesema ni muhimu elimu ya unasihi ikawa inatolewa kwa mabinti wanaorejea shuleni ili kukabiliana na vitendo vya unyanyapaa wanavyokutana navyo.
Amesema pia iko haja ya kuwepo mijadala itakayotengeneza kanuni zitakazolinda haki za wasichana wanaorejea shule baada ya kujifungua na kukemea vitendo vya unyanyapaa dhidi yao.
Akizungumzia hilo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dk Franklin Rwezimula amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha lengo la kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo linafanikiwa.
“Serikali imeshatoa mwongozo, changamoto ninayoiona hapa ni baadhi ya watekelezaji wa mwongozo huo kutokuwa na uelewa wa nini wanachotakiwa kufanya, muhimu kila mmoja kufuata majukumu yake kama ilivyoainishwa,” alisema.
“Wadau wakiwemo Hakielimu waliofanya utafiti huu tuchukue jukumu la kuelimisha, kuanzia ngazi ya jamii, shule, kata kila mmoja aelewe anatakiwa kufanya nini kulingana na mwongozo. Msiache pia kuwafikia wenye stori nzuri, wapo wasichana wamerejea shuleni, wanaendelea na masomo na wapo waliofanya vizuri,” amesema.
Utafiti huo ulifanyika kwenye mikoa sita ukihusisha wilaya 12 ambazo ni Ilemela, Meru, Buchosa, Kigoma, Kasulu, Rungwe, Kongwa, Mlimba na Halmashauri za Miji ya Mbeya, Dodoma, Arusha na Ifakara.