Dar e Salaam. Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema kuanzishwa kwa Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (Tamisa), kutachagiza azma ya Serikali ya kuhakikisha utajiri wa madini yaliyopo nchini unawanufaisha wananchi sambamba na kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Mavunde ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 15, 2024 alipokuwa anazindua chama hicho.
Amesema Serikali inataka kuona kampuni za Tanzania zikijitosa katika kuanzisha viwanda na kutengeneza bidhaa muhimu katika kuchimba madini.
“Serikali inatoa kipaumbele katika uwekezaji wenye tija kupitia ajira za ndani na matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini,” amesema Mavunde.
Amesema lengo la Serikali ni kukuza ukuaji wa uchumi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Waziri Mavunde amesema juhudi hizo zitachangia pia kuleta ajira, kukuza ujuzi na ukuaji wa tasnia zinazohusiana na sekta ya madini kwa lengo la kukuza uchumi wa ndani.
“Nimeambiwa Tamisa imeanzishwa ili kutetea masilahi ya wasambazaji katika sekta ya madini, kuboresha maudhui ya ndani, kuimarisha mazingira ya biashara, kukuza utamaduni wa uvumbuzi, ushirikiano kati ya wadau na uendelevu wa biashara ndani ya mfumo wa maudhui ya ndani,” amesema.
Hivyo, amepongeza dhamira ya Tamisa ya kutaka kuwaunganisha Watanzania katika sekta ya madini kupitia maudhui ya ndani.
Amesema sasa wasambazaji wa sekta ya madini wana sauti rasmi katika masuala muhimu jambo litakalosaidia kulinda haki zao na kuimarishwa kupitia uboreshaji wa mazingira ya biashara na utatuzi wa changamoto zao.
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Tamisa, Peter Kumalilwa amesema chama hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wasambazaji wa sekta ya madini, kutetea masilahi yao na kuimarisha mazingira ya biashara.
“Malengo yetu makuu ni pamoja na kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia,” amesema Kumalilwa.
Amesema lengo lingine ni kuendesha uvumbuzi na uendelevu sambamba na kuweka wanachama wao kama viongozi katika tasnia ya madini