MABAO matano waliyofunga katika mechi mbili za kirafiki, yameipa jeuri Mbeya City, huku kocha mkuu wa timu huyo, Salum Mayanga akieleza kasi hiyo ndiyo anaitaka watakapoianza Championship.
Mbeya City inatarajiwa kufungua pazia ya ligi hiyo Ijumaa ya wiki hii, Septemba 20 kuwakaribisha Big Man (zamani Mwadui) iliyoweka makazi yake mkoani Lindi, mechi ikipigwa Sokoine jijini hapa.
Timu hiyo ambayo ilishuka daraja misimu miwili iliyopita, katika mechi mbili ilizocheza za kirafiki imefunga mabao matano, ikianza dhidi ya Real Nakonde (Zambia) bao 1-0 na juzi ikaichapa 4-0 Hausung ya First League.
Mayanga alisema kwa sasa anaona uelekeo mzuri na kasi hiyo anaitaka iwe endelevu katika Championship ili kurejea Ligi Kuu na wako tayari kwa mapambano.
Alisema anafahamu Championship ni ngumu na hawataki kuona wanarudia makosa kama msimu uliopita hadi kushindwa kufikia malengo na kila mechi kwao itakuwa vita ya pointi.
“Vijana wameonyesha kitu chenye matumaini, tunataka kasi waliyoonyesha katika maandalizi iwe endelevu kuanzia mchezo wa kwanza dhidi ya Big Man, msimu huu hatutaki kurudia makosa,” alisema Mayanga.
Kuhusu ratiba, kocha huyo alisema haiko vibaya sana na kama watacheza kwa mahesabu ni wazi City inaweza kurudi tena wanapohitaji akiomba sapoti ya wadau na mashabiki.
“Ratiba siyo mbaya, kimsingi ni utayari wetu kuhakikisha kila mechi tunapata ushindi, hii ni ligi yeyote ana malengo yake, sapoti ya mashabiki ni muhimu sana,” alisema kocha huyo.