Operesheni ya kupambana na ugaidi yashika kasi

Miezi miwili baada ya jeshi la Pakistan kuanza operesheni ya kukabiliana na ugaidi, bado mashambulizi ya kigaidi katika baadhi ya maeneo yameripotiwa nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Pak ya mafunzo ya amani (Pips) inaeleza kuwa mashambulizi 59 yameripotiwa nchini humo mwezi Agosti mwaka huu ikilinganishwa na mashambulizi 38 mwezi Julai, mwaka huu.

‘’Takwimu za hivi karibuni zinaonesha Jeshi la Pakistan linapambana na wanaotekeleza matukio hayo. Hadi hivi sasa zimetengwa Dola milioni 300 kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi maeneo ya Balochistan na Khyber Pakhtunkhwa.’’

‘’Kati ya matukio 59 ya ugaidi, 29 yalitokea Khyber Pakhtunkhwa, 28 Balochistan na mawili huko Punjab na kusababisha vifo vya watu 84 na 166 kujeruhiwa,’’ zinaeleza takwimu za Pips.

Juzi, mkuu wa taasisi ya Jamiat Ulema-i-Islam-Fazl (JUI-F), Maulana Fazlur Rehman alilitaka Bunge la nchi hiyo kukutana na wananchi na viongozi wa Balochistan na Khyber Pakhtunkhwa ili kujadili kwa pamoja kukomesha matukio hayo.

Wawakilishi kutoka vyama vingine vya siasa pia walikutana na viongozi wakuu wa  serikali  kujadili suala hilo huku Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif akilitaka jeshi kuanzisha mazungumzo ya amani na makundi yenye itikadi kali na wanaharakati wa haki za binadamu kutoka makabila madogo ya Baloch na Pashtun.

Katika Mkutano wa hivi karibuni mmoja wa makamanda wa jeshi, alieleza jinsi jeshi la nchi hiyo linavyoungwa mkono  na kamwe halitaruhusu matukio ya ugaidi kuendelea.

Related Posts