MEI MOSI 2024; Kikokotoo kufanyiwa uchambuzi, nyongeza mishahara kutangazwa karibuni

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imesema imepokea hoja ya wafanyakazi kuhusu kubadilisha kikokotoo na kuahidi kukifanyia uchambuzi zaidi.

Aidha imesema itaendelea kuhuhisha viwango vya mishahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi wa utendaji wa waajiriwa.

Hakikisho hilo limetolewa leo Mei Mosi,2024 na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika kitaifa jijini Arusha.

Amesema uamuzi wa kubadilisha kikokotoo ni lazima utokane na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu bima hivyo wanategemea wataalam hao watashauri kuhusu uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kulitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

“Tunawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu anayependa kuona watu waliotumikia nchi hii wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao. Ndiyo maana Serikali ilichukua uamuzi wa kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii shilingi trilioni 2.147 hatua ambayo imeimarisha mifuko,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango amesema wanatambua umuhimu wa kupunguza ugumu wa maisha ya wananchi wote wakiwemo watumishi ndiyo maana mwaka 2022/2023 kima cha chini cha mshahara kiliongezwa kwa asilimia 23.3 kutoka Sh 300,000 hadi Sh 370,000 kwa mwezi ili kuwezesha watumishi wenye mishahara hiyo kumudu gharama za maisha.

“Tathmini ya ndani na iliyofanywa nje hivi karibuni imeonyesha nchi yetu inakopesheka na ina mvuto wa wawekezaji kutoka nje hivyo, endapo hali hii itadumu wafanyakazi wawe na matumaini kwamba tutasema jambo hivi karibuni,” amesema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango akizindua Gazeti la Mfanyakazi Tanzania wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha Mei 01, 2024. Kushoto ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya.

Amesema pia kwa mwaka 2024/25 wametenga Sh bilioni 252.7 kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi 219,924.

Amesema kuanzia Julai 2024 watumishi 473 katika halmashauri 191 wataanza kulipwa mishahara kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya halmashauri zao kubainika kutokuwa na uwezo wa kulipa kupitia katika mapato yake ya ndani ambapo Sh bilioni 3.5 zimetengwa.

Makamu wa Rais amesema pia kipindi cha uangalizi maalumu kwa watoto njiti hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi na mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 mchana kwa miezi sita ili kwenda kunyonyesha mtoto.

Amesema watafanya tathmini kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu kuhusu kuirejesha iliyokuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Dk. Mpango amesema hadi sasa Serikali imeridhia mikataba minane kati ya 10 ya msingi na imeanza mchakato wa kuridhia mikataba sita ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na kusisitiza kuwa uamuzi unafanyika baada ya kujiridhisha masuala ya msingi kama vile mila, desturi na tamaduni.

MAJALIWA

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) ambayo huadhimishwa kila mwaka ni siku maalum kwa ajili ya wafanyakazi kutafakari na kutathmini namna walivyotekeleza malengo waliyojiwekea katika mwaka husika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wafanyakazi wote duniani kuweka mipango kwa ajili ya mwaka unaofuata na ndiyo maana inafanyika kipindi ambacho nchini nyingi duniani zinakuwa katika maandalizi ya Bajeti.

“Siku hii ni muhimu sana na inatukumbusha wajibu wetu wafanyakazi wa kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo katika utendaji wetu wa kazi na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja na hatimaye kuleta tija katika maeneo ya kazi,” amesema.

HOJA ZA TUCTA

TUCTA kupitia Katibu Mkuu wake, Hery Mkunda, liliwasilisha hoja kadhaa ikiwemo ya kikokotoo na kusema wafanyakazi hawaridhishwi na matokeo ya kanuni mpya.

“Tunaomba kanuni za ukokotoaji mafao ziboreshwe kuleta mafao bora kwa wastaafu bila kuathiri uhai wa mifuko. Utaratibu wa sasa haukidhi malengo yaliyokusudiwa kwa kuwa Serikali ni mdhamini wa mifuko hivyo, haiwezi tena kuwa msimamizi na mdhibiti wa mifuko,” amesema Mkunda.

Aidha amesema maboresho ya mishahara hayajakidhi hali ngumu ya maisha iliyopo na kusababisha wafanyakazi kushindwa kukidhi mahitaji yao ya msingi na familia zao.

Shirikisho hilo pia limeomba migogoro ya kikazi itatuliwe kwa weledi na haraka kwani utaratibu uliopo sasa ni mrefu unasababisha wafanyakazi kutopata haki zao kwa wakati.

Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri (ATE), Oscar Mgaya, ameshauri tozo ya kuongeza ujuzi (SDL) iendelee kupunguzwa hadi kufikia asilimia mbili.

Amesema pia Serikali iliongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma na binafsi na wao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha waajiri wote wanafuata sheria na kuitekeleza.

Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugala, ametoa wito kwa serikali kuendelea kushughulikia kwa umahiri kipaumbele cha maendeleo ya kimataifa ambacho ni uzalishaji wa ajira hasa kwa vijana.

Aidha, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ‘Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mfano bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha’ inakwenda sambamba na taarifa za ILO katika nyanja ya ajira na mtazamo wa kijamii ya mwaka 2024.

Waziri wa Nchi (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndenjembi, amesema wataendelea kuimarisha utatu kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi na waajiri katika kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi na kuimarisha mahusiano mahala pa kazi.

Related Posts