Bikoko asimamishwa, arejesha tena Tabora Utd

KOCHA wa Tabora United, Mkenya Francis Kimanzi hataki utani baada ya kudaiwa kumsimamisha kwa kosa la utovu wa nidhamu beki wa timu hiyo, Andy Bikoko kabla ya kumsamehe na kumrejesha tena kikosini.

Kocha huyo ambaye ni muumini wa kusimamia nidhamu hasa kwa wachezaji wanaojaribu kutoka nje ya mstari, wanakumbana na adhabu zake na Bikoko ambaye ni raia wa DR Congo ameonja joto ya jiwe.

Ingawa ilifanywa siri, lakini habari za ndani kutoka  timu hiyo ni beki huyo alijikuta akiingia katika 18 za Kimanzi na kupewa adhabu ya kusimamishwa baada ya kutoungana na wenzake kambini mara walipoifunga Kagera Sugar bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Mwanaspoti lilipata taarifa za ndani, inadaiwa mchezaji huyo alilala nje ya kambi, hivyo kocha akaamua kumnyoosha kwa kumsimamisha, ili iwe fundisho kwa wengine, kabla ya kuomba msamaha na kusamehewa siku chache zilizopita.

“Baada ya kumalizika kwa mechi na Kagera, Bikoko hakupanda basi la timu, akaondoka na bodaboda, ingawa haikujulikana alikwenda wapi, baada ya kurejea asubuhi kocha akamhoji na kuona anastahili adhabu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Kocha hajali ukubwa wa jina la mchezaji, anataka wote watambue wapo kwa ajili ya kutimiza malengo ya Tabora United, hapendi kabisa kuona wachezaji wanakosa nidhamu, anajua akiruhusu hayo utakuwa mwanzo wa kufeli.”

Mwanaspoti liliamua kumtafuta Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala ambaye aliruka kimanga taarifa hiyo kwa kusema; “Hakuna mchezaji aliyepewa adhabu kama hamkumuona dhidi ya Prisons, hakuwa katika mpango wa kocha, mtamuona michezo mingine, Bikoko yupo kambini, kungekuwa na tukio hilo klabu ingetoa taarifa.”

Hata hivyo, pamoja na ofisa habari kutoa majibu hayo, taarifa ambazo Mwanaspoti ilihakikishwa ni beki huyo aliomba radhi kwa kocha kwa alichokifanya na Kimanzi amemsamehe na sasa ameungana na wenzake tayari kwa maandalizi ya mechi zijazo za Ligi Kuu iliyofikia raundi ya nne sasa.

Related Posts