WAWEKEZAJI BINAFSI KICHOCHEO KATIKA MAPINDUZI NA USHINDANI WA SEKTA YA ELIMU -RAS MCHATTA

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

SERIKALI  Mkoa wa Pwani ,imetoa rai kwa wawekezaji binafsi katika sekta ya elimu kuzingatia sheria katika ujenzi wa miundombinu bora na kuajiri walimu wenye sifa na vigezo ili kuchochea Mapinduzi makubwa katika sekta hiyo.

Aidha, Serikali ya mkoa huo imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji wanaowekeza katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari, lengo likiwa kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya sayansi na teknolojia ya kisasa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS) Rashid Mchatta, alitoa rai hiyo Septemba 14 wakati akizungumza na wazazi,walezi, wanafunzi,walimu na uongozi wa shule za Kibaha Independence Schools(KIPs), zinazomilikiwa na Yusuph Mfinanga (Njuweni Investment) kwenye mahafali ya 19 .

“Serikali ya Mkoa inatathimi mchango wa sekta binafsi katika kuboresha sekta ya elimu ,na hadi sasa kufikia 2024 mkoa una shule 774 kutoka shule 691 mwaka 2021 ambapo kati ya shule hizo 142 ni shule binafsi “alifafanua Mchatta.

Vilevile akiongea kuhusu maadili, aliwaasa vijana na wanafunzi kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa yao badala ya kujifunza mambo yanayodidimiza maadili ya kitanzania.

Kadhalika Mchatta aliwataka wazazi na walezi ,kusimamia na kudhibiti mienendo ya watoto wao waliohitimu elimu ya msingi ili kuwaepusha kutumbukia kwenye wimbi la mmomonyoko wa maadili na ukatili dhidi yao.

Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Njuweni Investment Ltd, alhaj Yusuph Mfinanga aliwashauru wazazi kujenga tabia ya kutenga bajeti kwa ajili ya kusomesha watoto ili kuondokana na usumbufu wakati wa kulipa ada

Mfinanga aliwataka ,wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi katika shule ya Main Kips,Annex na Msangani Kips kwenda kuendeleza maadili mema waliyopata shule.

Nae Kaimu Ofisa Elimu ,Halmashauri ya Mji Kibaha ,ambae ni Ofisa Taaluma Adrian Livamba aliwataka wamiliki shule binafsi, kuhakikisha wanazingatia weledi na taaluma kwa walimu wanaowaajiri na kuepuka kuajiri walimu wasiokuwa na taaluma ya ualimu.

Kuhusu mtihani wa Elimu ya Msingi, Livamba alisema halmashauri hiyo ina shule 71 kati ya hizo 29 ni binafsi ambapo wanafunzi 6,250 wamefanikiwa kufanya mtihani huo na hakukuwa na changamoto yoyote iliyojitokeza.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa KIPS Msangani ,Ramadhan Hussein alisema shule za Kips znarekodi nzuri ya ufaulu ndani ya miaka mitatu mfululizo wameshika nafasi ya juu kiwilaya na mkoa, na kuongeza waliohitimu elimu ya msingi ni wanafunzi 154.

Alitaja baadhi ya changamoto wanayokabiliana nayo kuwa ni ubovu wa barabara za mitaa Kidenge,ambazo wakati wa mvua zinasababisha uharibifu wa magari ya shule.

Hussein aliiomba serikali na halmashauri ,kusaidia kuboresha barabara za ndani za mitaa ili kuimarisha miundombinu ya barabara ziweze kupitika kirahisi.

Mwakilishi wa wazazi, Emmanuel Kulaya aliwashukuru walimu kwa kuwatunza na kuwapa elimu bora watoto wao kwani walimu wanajitoa kulea watoto kwa kiasi kikubwa.

Related Posts