KOCHA mpya wa Azam FC, Rachid Taoussi ameanza na suluhu katika Ligi Kuu Bara akiiongoza kwa mara ya kwanza dhidi ya Pamba Jiji, huku akisema hana presha na matokeo hayo na mambo mazuri yatakuja haraka.
Azam ilicheza mechi ya pili jana usiku ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi shukrani zikienda kwa mwamuzi Tatu Malogo aliyelikataa bao sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho baada ya kutofautiana na mwamuzi msaidizi aliyekimbilia kati kuashiria ni bao.
Suluhu hiyo ni ya pili baada ya awali kubanwa na JKT Tanzania wakati timu ikiwa chini ya kocha Youssouf Dabo aliyetemeshwa kibarua na juzi usiku Taoussi raia wa Morocco aliiongoza mbele ya Pamba iliyopanda Ligi Kuu na kutoka sare ya tatu mfululizo ikiwa haijafunga wala kufungwa bao katika ligi hiyo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya mchezo huo, kocha Taoussi alisema Azam ilikosa matokeo mazuri pekee, lakini amevutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na kikosi hicho katika mechi hiyo ambayo ni ya kwanza kwake.
Taoussi alisema timu hiyo ilitengeneza nafasi nyingi, lakini wakashindwa kuzituma na hapo ndipo kazi yake itakapoanzia katika mechi ijayo.
“Tulicheza vizuri sana hasa kipindi cha kwanza, muda mrefu tuliutumia kwenye eneo la wapinzani, lakini kuna kitu kimoja tu hakikwenda sawa na ni ishu ya kutumia nafasi ambazo zingebadilisha mchezo,” alisema Taoussi na kuongeza;
“Kazi yetu itaanzia hapa lazima tuwe na uwezo wa kufunga mabao ili tufanye vizuri kwenye mechi zetu, ni kama wachezaji walikuwa na presha hivi wakipoteza umakini, tutalifanyia kazi ili turudi imara zaidi.”
Kocha huyo aliongeza mabadiliko na muundo wa kikosi hicho akiwaweka nje baadhi ya wachezaji na alisema, aliamua kuwapumzisha baada ya kutoka katika majukumu ya timu ya Taifa, huku wengine akitaka kuwasoma zaidi.
“Tulibadilisha kikosi, ni kweli lakini nadhani mliona kuna wachezaji wetu wametoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa na siku ni chache tu zilizopita hivyo tukaona tuwapumzishe kulingana na muda waliocheza huko,” alisema Touassi aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwamo Wydad Casablanca aliyeongeza;
“Ndani ya hilo pia tulitaka kuwapa nafasi wachezaji wote ili tuone uwezo wa kila mmoja, kwani mchezaji ana nafasi ya kuitumikia hii timu kama atakuwa anajituma kwenye mazoezi na hata kwenye mechi zetu.”