Dar es Salaam. Ikiwa zimepita siku tano tangu dunia iadhimishe siku ya kupinga na kuzuia kujiua, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa takribani watu milioni nne huwaza na kutamani kujiua kila mwaka, lakini miongoni mwao ni watu 800,000 hujitoa uhai.
Kila mwaka ifikapo Septemba 10 dunia huadhimisha siku hii ya kupinga na kuzuia watu kujiua.
Ripoti hiyo inaonyesha kitendo cha watu kujiua hutokea katika rika zote bila kujali umri na mwaka 2015, kujiua kulishika nafasi ya pili kwa vifo vyote duniani hasa kwa vijana wa miaka 15-29.
Hata hivyo, wataalamu wanataja vichochezi vinavyochangia mtu kujiua ni magonjwa ya sonona, huzuni iliyopitiliza, kujiona mwenye hatia na kuwa na magonjwa ya hofu kupitiliza na dalili zinazoambatana na hilo.
Matumizi sugu ya dawa za kulevya na pombe pamoja na hali ya kuona vitu ambavyo watu wengine hawavioni, kusikia sauti ambazo wengine hawazisikii pia kuwa na mkanganyiko wa mawazo na hisia.
Huenda sababu za watu kujiua zimeelezwa mara kwa mara, lakini je, unawezaje kumtambua mtu anayetaka kujiua. Wanasaikolojia na wanasosholojia wanasema kuna mambo ambayo ukiyaona mtu akiyafanya mara kwa mara huenda ikawa ni dalili ya kutaka kujiua, hivyo inakuwa rahisi kumpa msaada.
Mwanasosholojia, Dk Abunuas Mwami anasema kwa ujumla msongo wa mawazo ni sababu kubwa ya watu kufikia kujiua, lakini analaumu ubepari ambao umewafanya watu wafarakanishwe na jamii zao.
“Kabla ya ukoloni, jamii za Afrika zilikuwa pamoja, lakini sasa ubepari umefanya thamani ya mtu iwe katika vitu. Kama huna kitu thamani yako inapotea na hilo binadamu ameshindwa kulidhibiti kiasi kwamba watu wengi wanajiona wapowapo tu, hawana mamlaka na hilo limewafanya waonekane kama chombo cha kutumikisha zaidi,” anasema mstaafu huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Mwami anasema ubepari ambao umesababisha mtu kufarakanishwa na jamii yake umewafanya watu wengi kujiona hawana thamani na hivyo kukata tamaa ya maisha. “Mtu wa namna hii akipata tatizo dogo tu, huamua kujiua kwa kudhani hana thamani.”
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema miongoni mwa dalili za watu wanaotaka kujiua ni upweke. “Mara nyingi watu wanaofikiria kujiua huwa wanakwepa mwingiliano na watu wengine, hupenda kuwa wenyewe wakitafakari, wanapima uamuzi wanaotaka kuuchukua kama ni sahihi au si sahihi,” anasema Modesta.
Miongoni mwa dalili kubwa ya mtu anayetaka kujiua ni kukata tamaa kwa kudhani wametengwa na jamii zao au dunia kwa ujumla. Watu wanaoonekana wamekata tamaa hawatakiwi kuachwa wenyewe, kwani wapo kwenye hatari ya kujiua.
Mwanasaikolojia wa zamani wa Ufaransa, Emile Durkheim katika tafiti zake aligundua kuwa watu wanapodhani wametengwa kutokana na mabadiliko ya ghafla ama ya kijamii, kisiasa au kiuchumi huchanganyikiwa na kukataa tamaa hivyo kujiua.
Pia imeelezwa watu wanaofikiria kujiua huwa hawataki kufikiria mambo ya mbele, hata kwa mambo ambayo tayari waliyapanga huwa wanaahirisha bila sababu ya msingi na wengine huahirisha hata safari muhimu.
Modesta anasema watu waliowahi kubakwa, pia wasipopata ushauri wa uhakika huwa kwenye hatari kubwa ya kujiua.
Sababu kubwa huwa ni kuona wamedharauliwa, wamedhalilishwa na zaidi wametengwa na kuonekana hawafai mbele ya jamii. Huwa na uwezekano wa kujiua kwa sababu ya kudhani kwa kufanya hivyo watakuwa salama zaidi.
Modesta anasema sababu nyingine ambayo huwaonyesha dalili za watu wanaotaka kujiua ni hasira na upweke na kwa mazingira yaliyopo ni rahisi watu waliowahi kubakwa kuwa na hasira na jamii na hata mara nyingi kuwa wapweke.
Mengine ni pamoja na kuandika wosia, mtu aliyewahi kutaka kujiua, anaona aibu na kutoangalia watu usoni.
“Watu hawa huwa wanatafakari mara kwa mara kama wanachokifanya ni kosa au si kosa, hujiona wakosaji,” anasema Modesta.
Wanaopenda kuzungumza kuhusu masuala ya kujiua au kuua watu wengine, baadhi huwa wanazungumza kama masihara huku wakisema wanataka kujidhulu au hawapendi kuishi duniani.
Wanasaikolojia kwa pamoja wanakubaliana kuwa watu wa kundi hili huwa wakipata tatizo kidogo na likachochea hasira zao, huwa wanajiua na hasa wanapoachwa pekee yao bila familia au marafiki. Inashauriwa kuwa mtu anayezungumza mara kwa mara kuhusu mauaji asiachwe mwenyewe.
Profesa wa uchunguzi wa magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Columbia Medical Center kilichopo New York, Marekani, Madelyn Gould anasema hali ya kujiona mkosaji inapozidi, ambayo huwa ni dalili ya msongo wa mawazo na hofu, ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa karibu na mtu akiwa na dalili hizo anapaswa asiachwe peke yake.
“Unaanza kudhani ni mkosaji kuhusu jambo fulani, unadhani umewaangusha wenzako. Ukizungumza na mtu mwingine anakwambia hujafanya kosa kubwa, lakini huamini,” anasema Gould.
Dk Mwami anasema mtu mwenye msongo wa mawazo ambayo yametokana na kufarakanishwa na jamii yake, hujiona dhaifu na asiye na mamlaka yoyote, hivyo huanza kujiona mkosaji katika jamii yake.
Mkurugenzi wa taasisi ya Marekani ya kuzuia watu kujiua, Dk Paula Clayton anasema matumizi ya dawa za kulevya na kunywa pombe kupita kiasi, mambo ambayo baadhi ya watu hutumia kama kupunguza mawazo au hasira ni ishara za mtu anayetaka kujiua.
Kuwa na silaha nyumbani, matatizo ya kiafya, matumizi ya kompyuta/simu pia ni dalili nyingine ambayo inaweza kuonyesha kuwa mtu anataka kujiua.
“Ukiangalia watu wengi waliojiua ukienda kwenye kompyuta zao utagundua mara kwa mara walikuwa wakitafuta kwenye google jinsi ya kujiua,” anasema Dk Clayton huku akishauri wazazi kuwafuatilia watoto wao hasa kwenye Facebook na mitandao mingine kama simu.
Maumivu yanayotokana na msongo wa mawazo au sonona na magonjwa ya akili pia ni kichocheo kikubwa cha watu kujiua.
“Sonona ni ugonjwa unaoongoza watu kujiua, kwa hiyo mtu anapopata sonona kali, ndivyo anavyokuwa na ukaribu zaidi wa kujinyonga. Mtu anapokatishwa tamaa anakuwa hatarini zaidi kujiua,” anasema Dk Clayton.
Wakati kujiua kunachukuliwa kama kosa la jinai. Chini ya Kanuni ya Adhabu ya 216&217 yaani penal code 216 &217, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Michelle Chapa Foundation, Dk Michelle Chapa anasema kujitoa uhai ni tatizo la afya ya akili, sio kosa la jinai.
“Kujitoa uhai yaani ‘suicide’ ni dalili ya matatizo ya afya ya akili na sio kosa la jinai. Siyo chaguo mtu anaamua kufanya, mara nyingi ni matokeo ya matatizo ya afya ya akili yasiyotibiwa,” anasema.
Dk Chapa anasema matatizo hayo kama vile unyogovu yaani ‘depression’, kiwewe kwa maana ya ‘trauma’ na dhiki kali ya kihisia yaani ‘severe emotional distress’ humuathiri mtu kiafya na si tabia za jinai, watu wanapojaribu kujitoa uhai wao si wahalifu, bali wanahitaji msaada wa haraka na uelewa.
Anasema matokeo ya kuweka jinai kwenye kujitoa uhai, huleta changamoto kubwa kwa watu wanaohitaji msaada wa afya ya akili, maana inaendelea kudumisha unyanyapaa.