Goran ambeba Yona, alili bao Chamazi

PAMBA Jiji bado inaendelea kujitafuta baada ya kurejea Ligi Kuu ikiwa imepita miaka 23 tangu iliposhuka daraja, lakini kocha wa timu hiyo, Goran Kopunovic akimtaja kipa Yona Amos kama mchezaji aliyesaidia timu hiyo kuwa imara hadi sasa katika ligi hiyo, licha ya kutopata ushindi wowote.

Timu hiyo hadi sasa haijafunga bao lolote wala kuruhusu wavu wake kuguswa katika mechi tatu zilizopita, huku Yona aking’ara kwa kuokoa mikwaju iliyoinusuru timu hiyo na kuchaguliwa mara mbili kuwa nyota wa mchezo katika mechi za Azam na Tanzania Prisons.

Kiwango cha kipa huyo kwenye mechi tatu akiwa na timu yake kimekuwa mwiba mkali kwa timu pinzani na kocha Goran amefunguka namna kipa wake anavyowabeba.

Goran aliliambia Mwanaspoti, uwepo wa Yona kwenye ukuta wao ni wa muhimu kwani ni mchezaji aliyeisaidia timu hiyo kurudi mchezoni wakati anaelemewa kutokana na uwezo wake wa kuokoa.

Kocha huyo raia wa Serbia alisema wakati timu yake ikiendelea kupambana juu ya kufunga mabao bado wamekuwa imara kuhakikisha hawaruhusu nyavu zao kutikiswa.

“Hakuna timu ambayo imemaliza ligi ikiwa haijawahi kufunga bao au kupata matokeo ya suluhu, naamini mambo yatabadilika hivi karibuni tutaanza kufunga,” alisema Goran kocha wa zamani wa Tabora United na Simba na kuongeza;

“Tunafanya juhudi kubwa ili tuweze kufunga mabao, angalia leo (juzi) tumefunga bao, lakini waamuzi wetu wameona halikustahili ingawa nimeongea na watu mpaka Canada wanashangaa kwa nini limekataliwa.

“Kuhusu Yona nadhani kila kitu kimeonekana ni mmoja kati ya vijana wetu bora tulionao kwenye timu, kuna wakati kikosi chetu kinakuwa chini kimchezo, lakini amekuwa imara kukirudisha mchezoni, nadhani atakuja kuwa tegemeo wa taifa hili siku sio nyingi.”

Related Posts