Dar Lux yaamuriwa kurejesha Sh18 bilioni ya Equity, riba

Dar es Salaam. Kampuni ya Dar Lux  imeamuriwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kurejesha mkopo iliouchukua kutoka Benki ya Equity Tanzania Limited (EBT) ambao ni zaidi ya Sh18.93 bilioni, baada ya kukaidi kuurejesha.

Pia imeamuriwa kulipa riba ya asilimia 10 ya kiasi hicho kwa mwaka kuanzia tarehe iliyotakiwa kurejesha mkopo huo mpaka tarehe ya EBT kufungua kesi  na riba ya asilimia saba kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kumaliza malipo yote.

Vilevile imeamuriwa kuilipa EBT, Sh10 milioni kama fidia ya madhara ya jumla kwa kushindwa kurejesha mkopo huo, pamoja na gharama za uendeshaji kesi hiyo.

Amri hiyo imetolewa na Mahakama  katika hukumu ya kesi ya kibiashara namba 02 ya mwaka 2023 iliyofunguliwa na EBT dhidi ya kampuni hiyo inayojishughulisha na utoaji wa huduma za usafiri wa mabasi pamoja na wenzake watatu.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Simagunga General Trading Co. Limited, Donald Xavery Simagunga na Pendo Donald Xavery, ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Dar Lux na pia wadhamini wake katika mkopo huo.

Hukumu ya kesi ya Dar Lux, iliyotolewa na Jaji  Cleophace Morris, Agosti 30, 2024, kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2016 na 2022 EBT iliikopesha kampuni hiyo kwa ajili ya shughuli zake za kibiashara.

Pamoja na hati za mali zilizowekwa na kampuni hiyo kama dhamana ya mkopo huo, pia ilikuwa na udhamini binafsi wa kampuni Simagunga General Trading, na wakurugenzi wake, Donald Simagunga na Pendo Donald.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilikiuka mkataba wa mkopo huo baada ya kushindwa kurejesha kwa muda waliokuwa wamekubaliana.

Hata baada ya kuiandikia notisi kampuni hiyo pamoja na wadhamini wake ya kuwataka walipe mkopo huo, lakini bado hawakutekeleza, ndipo benki hiyo ikaenda mahakamani.

Katika hati yake ya madai na katika ushahidi wake EBT ilidai mpaka wakati inafungua kesi hiyo deni lilikuwa limefikia zaidi ya Sh20.98 bilioni.

Hivyo EBK iliiomba Mahakama itamke kuwa mkopaji na wadhamini wake wamekiuka makubaliano ya mkopo  na iwaamuru walipe zaidi ya Sh20.98 bilioni.

Pia iliomba ilipwe riba ya asilimia 18 kwa mwaka inayotozwa kila mwezi kuanzia siku ya kwanza ya ukiukwaji wa makubaliano mpaka tarehe ya hukumu, fidia ya madhara ya jumla na gharama za kesi pamoja na gharama za kudai deni hilo.

Benki hiyo pia iliomba Mahakama itoe amri ya kukamata na kupiga mnada mali zilizowekwa dhamana na wadaiwa kufidia deni hilo.

Benki hiyo ilidai ukiukwaji huo wa makubaliano uliofanywa na mkopaji na wadhamini wake uliisababishia hasara mbalimbali kama vile kukosa kiasi cha pesa kinachodaiwa, kushindwa kuwekeza.

Nyingine ilidai ni kutafuta fedha mbadala kukidhi majukumu ya kila siku ya kifedha na gharama za kufuatilia kurejeshewa kwa deni hilo.

Kesi hiyo ilisikilizwa na kuamuriwa wa upande mmoja baada ya wadaiwa kutotokea kwenye hatua ya usuluhishi na hivyo maelezo yake ya utetezi wa maandishi kujibu hati ya madai yametupiliwa mbali, mdai akaendelea kuthibitisha kesi yake bila uwepo wa wadai.

Katika kuthibitisha madai yake EBT ambayo iliwasilishwa na mawakili Elly Mkwawa na Gilbert Masaga ilimuita shahidi mmoja tu, Ibrahim Mavika, ambaye kwa kiasi kikubwa ushahidi wake ulifafanua yaliyokuwamo kwenye hati ya madai.

Jaji Morris katika hukumu yake baada ya kusikiliza na kuchambua ushahidi huo wa upande wa mdai amekubaliana na mdai kuwa amethibitisha wadaiwa wamekiuka mkataba wa mkopo na wameingia hasara.

Amesema mdai katika madai yake ya deni amethibitisha  kiasi cha Sh18,939,022,800.75 (zaidi ya Sh18.9 bilioni) badala ya Sh20,981,468,221.12 (20.98 bilioni) alizodai kwenye hati ya madai.

Hivyo amesema Mahakama imeridhika mdai amepata hasara ya kukosa kiasi hicho  cha pesa (deni hilo) lakini akakataa madai ya hasara nyingine zilizotakwa kwenye hati ya madai akisema kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa kuhusiana na gharama zinazohusiana na deni hilo.

“Vivyohivyo, hakuna ushahidi kwenye kumbukumbu wa namna gani mdai ameshindwa kutumia kiasi hicho cha deni katika uwekezaji. Pia hakuna ushahidi wa gharama za kufuatilia deni hilo,” amesema Jaji Morris.

Kuhusu malipo ya riba Jaji Morris amesema kuwa kulinga na mazingira ya kesi hiyo anatoa riba ya asilimia 10 (badala ya 18), ya kiasi cha deni hilo kwa mwaka inayohesabiwa kuanzia tarehe ya ukiukwaji wa malipo hayo mpaka tarehe ya hukumu hiyo.

Jaji Morris amekataa madai mengine ya EBT kuhusu baadhi ya nafuu ilizoziomba na hasara ilizodai kuzipata akieleza kuwa ilishindwa kuthibitisha.

Related Posts