Serikali ilivyovuna mabilioni faini za barabara, mali za Sh2.3 bilioni zikitaifishwa

Dar es Salaam. Ripoti ya uhalifu na makosa ya usalama barabarani ya mwaka 2023 imebainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeingiza zaidi ya Sh3.82 bilioni kupitia faini mbalimbali zilizolipwa mahakamani.

Kiasi hicho cha fedha kimekusanywa kutokana na makosa mbalimbali, huku sekta zinazohusiana na mazao ya misitu, nyara za Serikali na usalama barabarani zikiongoza. Pia, mali zenye thamani ya Sh2.313 bilioni zilikamatwa na kutaifishwa na Serikali katika kipindi hicho.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha faini kubwa zaidi zililipwa na watuhumiwa waliokutwa na mazao ya misitu na jumla ya Sh1.492 bilioni zililipwa kama faini.

Nyara za Serikali zilishika nafasi ya pili na faini za Sh961.18 milioni zililipwa. Kwa upande mwingine, faini za makosa ya usalama barabarani zilifikia Sh398.76 milioni, huku makosa mengine yakichangia Sh337.98 milioni kama faini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Jeshi la Polisi limeeleza makosa ya kukutwa na nyara za Serikali yanasababishwa na tamaa ya watu kujipatia kipato isivyo halali pamoja na kukosa maadili.

Sababu nyingine zinatajwa kuwa ni pamoja na mazingira magumu ya kijamii na kiuchumi, kuathiriwa na makundi yasiyofaa, uhaba wa ajira na uwepo wa bandari bubu na njia haramu katika maeneo ya mipakani.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa kwa kushirikiana na nchi jirani, linaendelea kufanya operesheni za kukabiliana na wahalifu wa ndani na nje ya nchi. Vilevile, kumekuwa na jitihada za kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni, na kuendeleza doria za mara kwa mara katika maeneo ya mipakani na bandari bubu.

Pia, ushirikishwaji wa wazazi na walezi katika familia, shule, na vyuo umeonekana kuwa muhimu kwa kutoa elimu ya maadili na uraia, ili kupambana na uharibifu wa mazingira na kulinda rasilimali za Taifa.

Hii inajumuisha kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira.

Mhifadhi mkuu wa kitengo cha operesheni kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa), Mark Chuwa amezungumza na Mwananchi juu ya hili na kusema wameendelea kushirikiana na wananchi katika kupambana na ujangili na biashara haramu ya nyara za serikali.

Amesema watu wanatoa taarifa za uhalifu zinazosaidia kuendesha doria na operesheni dhidi ya wahalifu, huku wakitegemea taarifa za kiintelijensia.

“Mamlaka inaendesha doria za kushtukiza katika maeneo ambayo yamebainika kuwa na changamoto kubwa ya ujangili. Doria hizi zinasaidiwa na vitengo vya upelelezi na uendeshaji wa mashtaka, ili kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Hata hivyo, Chuwa amesema ushirikiano na kamati za usalama za mikoa na wilaya umeimarishwa, ili kutoa elimu kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa za uhalifu.

Meneja Uhusiano kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Johari Kachwamba naye amezungumzia mafanikio ya ukusanyaji wa faini nyingi yamechangiwa na uimarishaji wa doria katika misitu inayosimamiwa na TFS kwa kushirikiana na vyombo vya dola.

“Hata matumizi ya teknolojia nayo yamewezeshwa katika ufuatiliaji na ukamataji wa wahalifu, hii ni pamoja na matumizi ya drones kwa ajili ya doria za haraka,” amesema Kachwamba.

Amesema TFS imeendelea kuwekeza katika ulinzi wa misitu kwa kuhusisha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi pamoja na kuboresha vifaa vya usafiri na ulinzi kama vile magari makubwa na madogo, ili kuwezesha operesheni za ulinzi.

Kwa upande wa mali zilizotaifishwa, ripoti inaonyesha wanyama wa kufugwa walikuwa na thamani kubwa zaidi ya mali zilizotaifishwa, sawa na Sh638.699 milioni.

Dhahabu yenye thamani ya Sh409.778 milioni pia ilikamatwa, huku mali nyingine kama baiskeli za Sh3.2 milioni, pikipiki za Sh317.76 milioni na fedha taslimu za Sh62.97 milioni zikitaifishwa. Nyara za Serikali zenye thamani ya Sh328.93 milioni na mali nyingine zenye thamani ya zaidi ya Sh551.822 milioni pia zilikamatwa na Serikali.

Katika mipango ya baadaye, Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuendelea kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori.

Kupitia Bajeti ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2024/2025, wizara imeweka mikakati ya kupambana na ujangili na biashara haramu ya nyara, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mkakati wa kupambana na ujangili wa mwaka 2023/2033 na mkakati wa kusimamia na kuhifadhi tembo wa mwaka 2023/2033.

Mradi wa kupambana na ujangili unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (Global Environmental Facility – GEF), kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), pia utaendelea.

Mradi huo utatumia Sh3.66 bilioni kununua vifaa vya doria na kutoa mafunzo maalumu kwa maofisa wa usimamizi wa wanyamapori na misitu, ili kudhibiti ujangili na biashara haramu ya nyara nchini.

Related Posts