KAMPUNI ya Vodcell yaelekezwa kuilipa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu shilingi milioni 362 ndani ya siku saba ikiwa ni fedha za ushuru wa zao kwa Halmashauri hiyo.
Maelekezo hayo yametolewa na Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo akiwa kwenye ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkoani Shinyanga tarehe 15 Septemba 2024.
Aidha, Waziri Bashe amewaambia pia wananchi wa Ushetu wakati wa Mkutano wake wa hadhara na kuwaeleza kuwa Serikali itajenga visima katika vijiji 4 ambapo usanifu umeanza ili kujua wapi pa kuchimba visima. Vile vile, amesema kuwa usanifu na upembuzi yakinifu umeanza katika mradi wa Ziwa Victoria ili luweza kulaza bomba la kusambaza maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji kwa Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mara, Singida, Dodoma na mingine.
Ameomba kwa msisitizo kwa wanakijiji wa Mbika kuacha kujenga nyumba mabondeni ili kulinda ardhi za kilimo na umwagiliaji. “Tutajenga pia mabwawa na kutenga maeneo kwa ajili ya mifugo,” amesema Waziri Bashe.
Kuhusu Vyamva vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) vya Tumbaku vilivyopo chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tumbaku cha KACU, Waziri Bashe amewahamasisha wakulima wajisajili na kupeleka mahitaji yao ili wapatiwe mbolea ambayo inasambazwa na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).