Dar es Salaam ndio jiji kubwa nchini na mambo yake bila shaka ni makubwa. Hivi unajua kama majina ya mitaa na barabara kadhaa yanayotumika sasa katika jiji hilo sio ya asili?
Kazi hii inaangazia baadhi ya mitaa mitaa na barabara maarufu sambamba na majina yake ya kihistoria.
Sio jambo kubaini kuwa aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Samora Machel alitunukiwa mtaa huu na Serikali ya Tanzania kama sehemu ya kumuadhimisha.
Lakini wasichokijua wengi ni kuwa mtaa huo maarufu katika Jiji la Dar es Salaam, una historia ya kubadili majina mara kadhaa. Awali mtaa huo miaka ya 1880 ulijulikana kwa jina la asili ya Kihindi la Barra Rasta likimaanisha barabara kubwa, ukiwa mtaa mkubwa zaidi katika eneo hilo lililokuwa limejengwa na Sultan Majid.
Utawala wa Kijerumani ukabadilisha na kuuita Under de Acacien yaani mtaa ulio nchini ya miti ya mikesia.
Waingereza walipotawala baada ya vita ya pili ya dunia, wakauita kwa jina la Acacia Avenue. Hata hivyo jina hilo halikudumu sana kwani baada ya Tanzania kupata uhuru wake, mtaa ukabadilishwa na kuitwan Independence Avenue, kabla ya baadaye mwaka 1986 kuitwa Samora Avenue kama njia ya kumuenzi Rais huyo wa Msumbiji aliyepoteza maisha kwa ajali ya ndege.
Barabara hii iliyo kati ya makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Nyerere/ Nkrumah, zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Barabara ya UWT yaani Umoja wa Wanawake. Ilipewa jina la Bibi Titi ili kukumbuka na kuenzi mchango wa mwanamama huyo shupavu aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Alifariki mwaka 2000.
Tanzania haikuona ajizi kumpa Nelson Mandela barabara nchini ikiwa ni sehemu ya kumuenzi mpigania uhuru huyo na rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini.
Kabla ya Mandela kupewa barabara hiyo mwaka… awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Port Access linalomaanisha lango la bandari. Ilijengwa na iliyokuwa kampuni maarufu zamani ikiitwa Mowlem. Ni kwa sababu hiyo wapo waliokuwa wakiita barabara hiyo kwa jina la Mowlem.
Ikumbuke kuwa hii ndiyo barabara kuu inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam, mikoa na nchi jirani. Barabara hii inaanzia makutano ya Barabara ya Kilwa eneo la bandarini na kuishia makutano ya Barabara ya Morogoro, Ubungo.
Ndio barabara iliyo na lango kuu la nchi kwa kupitia usafiri wa anga yaani uwanja wa ndege. Kabla ya kuitwa kwa jina la Nyerere, barabara hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Pugu ambalo ni eneo la barabara hiyo kama unaelekea Wilaya ya Kisarawe. Inaanzia kwenye makutano ya Mtaa wa Gerezani Kariakoo.
Moja ya historia ya kuvutia ya mtaa huu ni kupakana na viwanja vya Mnazi Mmoja vyenye historia ya kipekee katika harakati za Uhuru. Awali ulijulikana kwa jina la New Street, lakini baada ya Uhuru Serikali iliubadilisha na kuuita Lumumba ikiwa ni sehemu ya kumuenzi mpigania uhuru maarufu wa Zaire, Patrice Lumumba.
Moja ya barabara maarufu inayounganisha katikati ya jiji na viunga vyake kama vile Ilala na Buguruni.
Kabla ya Uhuru, barabara hii ilijulikana kwa jina la Kichwele. Ni kandoni mwa barabara hiyo pia kuna shule ya Kichwele, inayotajwa kuwa shule ya kwanza ya msingi.
Si kubadilika kwa majina tu, lakini Jiji la Dar es Salaam lina sifa ya majina ya asili kufutika na kuchukua majina mapya.
Ipo hoja ya majina hayo kubadilika kwa wahusika kutaka kufuta aina fulani ya historia katika eneo husika au mabadiliko tu yanayofanywa na mamlaka..
Tunakuangazia baadhi tu ya maeneo ambayo majina ya asili yametoweka.
Ni kituo cha mabasi na eneo lililopo Kariakoo barabara ya Morogoro na Umoja wa Mataifa. Awali eneo hilo lilijulikana kwa jina la Mwembetogwa.
Kulikuwa na mti wa mbwembe na mtu akiuza togwa chini yake.
Hata hivyo baadaye kwa kuwepo kituo cha Jeshi la Zimamoto na uokoaji, jina la eneo hilo likabadilika na kuwa Faya kutoka jina laKiimgereza Fire, likiashiria jengo la jeshi hilo lililopo katika makutano ya barabara ya Morogoro na Umoja wa Mataifa mkabala na Shule ya Wasichana ya Jangwani.
Eneo ambalo sasa linajulikana kwa jina la Dar es Salaam, awali mji uliitwa Mzizima kabla ya Sultan Majid bin Said kutoka Zanzibar kulibadili jina eneo hilo na kulipa jina la Dar es Salaam likiwa na maana ya nyumba ya salama.
Ni eneo maarufu lililopo Kata ya Magomeni jijini Dar es Salaam. Awali eneo hilo linaelezwa kuwa lilikuwa likijulikana kwa jina la Magomeni Kisutu.
Kabla ya eneo hili kuchukua jina la Aziz Ali aliyekuwa mtoto wa mpigania uhuru maarufu, Dossa Aziz, awali lilijulikana kwa jina la Magogoni. Ni eneo lililopo Temeke jirani na viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya kibiashara pembezoni mwa Barabara ya Kilwa.
Kata hii iliyo katika Jiji la Dar es Salaam, ina historia ndefu katika chimbuko la jiji hilo tangu miaka ya 1800. Miaka hiyo Kivukoni ilijulikana kwa jina la Mbwa Maji ikikaliwa zaidi na watu wa jamii za Kibalawa na Kizaramo.