Fadlu aliamsha Simba, arudia jambo lile lile

KIKOSI cha Simba jana usiku kilikuwa jijini Tripoli, Libya kumalizana na Al Ahli Tripoli katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ameliamsha mapema kwa kutoa tamko ambalo mabosi na mashabiki wao wakisikia watachekelea.

Simba iliyoanzisha hatua hiyo, ilivaana na Al Ahli kwenye Uwanja wa Juni 11 kuanzia saa 2:00 usiku kabla ya kurudiana wikiendi hii Kwa Mkapa na mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa ngazi ya klabu baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Simba aliyekuwa akiiongoza kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo baada ya awali kuiongoza kwenye mechi za Ngao ya Jamii na Ligi Kuu, alisema kuanzia matokeo ya mchezo huo wa jana na mingine iliyopo mbele yake yanatakiwa kuwajenga kisawasawa kuhakikisha wanafanya makubwa Afrika.

Fadlu alisema kwa kikosi alichonacho kama wachezaji watakaza zaidi basi wana nafasi kubwa ya kufika kama sio nusu fainali basi ni fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu. Yanga ndio timu pekee ya Tanzania iliyocheza fainali ya Kombe la Shirikisho tangu michuano hiyo ilipobadilishwa na kuendeshwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2004, ikifanya hivyo msimu wa 2022-2023 ikilikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema malengo ya timu hiyo aliyopewa ni kuchukua ubingwa wa Afrika katika michuano ya kombe hilo na ameziangalia timu zinazowania taji hilo na kushtukia wanatakiwa kutunza heshima kwa kufika mbali, kwani njia ni nyeupe wakikaza buti zaidi.

Alichofanya Fadlu ni kuangalia msimamo wa klabu bora 10 Afrika na katika michuano hiyo zipo tatu tu, yaani Zamalek ya Misri inayoshikilia inayotetea taji, iliyopo nafasi ya tano, RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya sita kisha wao, Simba inayokamata nafasi ya saba. Berkane ilicheza fainali ya msimu uliopita na kupoteza mbele ya Zamalek ya Misri iliyotwaa taji hilo.

Kwa msimamo huo, Fadlu akaanza naye akipiga hesabu mapema akitaka kuona Simba lazima ipasue katikati ya vigogo hao ili icheze fainali ya shirikisho msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema amekaa na wachezaji akiwaambia kuanzia mchezo wa jana dhidi ya Al Ahly wanatakakiwa kuhakikisha hesabu zao zinakuwa sawasawa kwa kupata matokeo yatakayowafikisha mbali.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini alisema licha ya kwamba kikosi chake ni kipya, lakini kitaendelea kuboreshwa kwa umakini ili Simba ifikie malengo yenye hadhi yake Afrika.

“Ukiangalia orodha ya klabu bora Afrika, utaiona Simba nani yuko sawa na sisi au zaidi utawaona Zamalek na Berkane, hizi timu zote nazijua nazo zinajua ukubwa wa Simba. Tunahitaji kufikia malengo yetu kwa kuwa kati ya hizo timu mbili tucheze fainali ya shirikisho, wanaobeba dhamana hiyo ni sisi makocha na wachezaji wangu, tunatakiwa kuanzia hapa dhidi ya Al Ahly Tripoli,” alisema Fadlu na kuongea;

“Haijalishi timu hii ni mpya kwetu lakini tutaendelea kuiboresha kadiri ya muda unavyokwenda, tunatakiwa kuhakikisha tunashinda mechi moja kwenda nyingine tukifanikisha hili ndani yake Simba itaimarika na kuwa timu ngumu.”

Kauli ya Fadlu inachangiwa zaidi na uwepo wa mastaa wenye uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa kama straika, Steven Mukwala aliyetua hivi karibuni kutoka Asante Kotoko ya Ghana anayeng’ara pia timu ya taifa ya Uganda.

Kuna Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, makipa Mousa Camara, Aishi Manula na Ally Salim aliyeibeba timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi mbili za Kundi H kuwani kucheza fainali za Afcon 2025 dhidi ya Ethiopia ulioisha kwa suluhu na ile ya ushindi wa 2-1 mbele ya Guinea.

Pia kuna mabeki wa maana kama Chamou Karaboue, Abdulrazak Hamza, Che Fondoh Malone, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na viungo wanaojua kuilinda na kuindesha timu kama Mzamiru Yassin, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Yusuf Kagoma na wakali wengine ambao jana walitarajiwa kuliamsha mbele ya Walibya.

Rekodi ya Simba kucheza robo fainali tano katika misimu sita tofauti tangu iliporejea katika michuano ya kimataifa msimu wa 2028-2019 inaelezwa ni sababu nyingine inayomfanya kocha Fadlu kuamini kikosi hicho kina nafasi ya kufika mbali zaidi msimu huu.

Simba ilicheza makundi na kukwamia robo fainali msimu wa 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 kwa Ligi ya Mabingwa na 2021-2022 kwa Kombe la Shirikisho, kuonyesha ina uzoefu mkubwa.

Related Posts