Gofu Wanawake yaibeba nchi kimataifa

MCHEZO wa Gofu Tanzania umepiga hatua kubwa sana katika ngazi ya kimataifa huku  gofu ya ridhaa kwa wanawake ikitajwa kuwa na mafanikio zaidi ya ile ya  wanaume, ripoti ya Chama cha Gofu ya Wanawake nchini imethibitisha.

Akizungumza katika viwanja vya Arusha Gymkhana ambako michuano ya wazi ya Tanzania  iliingia siku yake ya  pili, Rais wa Chama cha Gofu ya Wanawake Tanzania(TLGU), Queen Siraki alisema mchezo wa gofu ni moja ya michezo michache nchini inayofanya vizuri kimataifa  na kusisitiza kuwa wanawake ndiyo wanaofanya vizuri zaidi hasa katika kitengo cha gofu ya ridhaa.

“Tumefanya vizuri na tunaendelea kufanya vizuri  na hivi sasa Watanzania saba wako katika kumi bora ya mashindano ya Tanzania Open yanayoendelea hapa Arusha,” alisema Queen.

Mashindano ya Tanzania Ladies Open pia yatatumika kama kipimo cha wachezaji kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya ubingwa wa Afrika nzima yatakayochezwa Morocco mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa matokeo ya mashimo 36 kati ya 54 ya michuano hii, Madina Idd ambaye anaongoza kwa upande wa Tanzania kwa alama ya mikwaju +16, Hawa Wanyeche mwenye +17 na Neema Olomi aliyekuwa na +25  hadi Jumamosi jioni, wako katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa katika timu ya taifa itakayocheza nchini Morocco.

Wengine ambao wanaweza kupata nafasi ni Aalaa Somji wa Arusha ambaye alikuwa na kiwango cha +32 katika nafasi ya sita na Vicy Elias aliyepata +38 akiwa wa saba.

Wote wa tano, kwa mujibu wa takwimu, pia walifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa nchini Ghana, Zambia, Kenya na Uganda  kwa kushinda, kupata nafasi ya pili au ya tatu.

Mwenye matokeo bora kabisa ni Madina Iddi wa Arusha ambaye aliiwezesha Tanzania kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Afrika kusini katika mashindano ya Afrika nzima yaliyofanyika mwaka 2018 katika viwanja vya Achimota nchini Ghana akishirikiana na Hawa Wanyeche.

Licha ya kushinda mataji katika michuano ya wazi ya wanawake nchini Ghana, Kenya, Uganda na Zambia, Madina na Wanyeche pia waliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Afrika nzima ambayo Tanzania iliyandaa mwaka 2022.

Madina Iddi pia ni Mtanzania wa  kwanza kushinda ubingwa wa  Afrika kwa wachezaji binafsi baada ya kumshinda Mwafrika ya Kusini mwaka 2018.

Tangu kuasisiwa kwa mashindano ya Afrika nzima mwaka 1992, ni Madina na Mkenya Rose Naliaka pekee ndiyo wana Afrika Mashariki waliowahi kushinda taji la Afrika kwa mchezaji binafsi.

Related Posts