Mwanga. Huzuni na majonzi vimetanda miongoni mwa mamia ya waombolezaji waliohudhuria katika Kanisa Kuu la Mwanga, Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, wakati mwili wa aliyekuwa Askofu wa dayosisi hiyo, Chediel Sendoro, ulipowasili kwa ajili ya ibada ya kuuaga.
Mwili huo kabla ya kufikishwa kanisani hapo, ulipelekwa nyumbani kwake eneo la Kileo, ambako wazazi wake na waombolezaji wengine walipata fursa ya kuuaga.
Baada ya kutolewa Kileo, mwili ulipelekwa katika makazi ya Askofu huyo Mwanga ambapo mkewe, familia na waombolezaji wengine walipata fursa ya kuaga na kisha kupelekwa Kanisa kuu Mwanga, ambapo itafanyika ibada ya kuaga.
Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9,2024 kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.
Historia inaonyesha kuwa Askofu Sendoro ndiye Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Pare.
Baadhi ya waumini na waombolezaji wameonekana wakishindwa kujizuia kulia wakati mwili huo ukiingizwa kanisani na wakati wakipita kutoa heshima za mwisho.
Akizungumza leo Septemba 16, 2024 wakati taratibu za kuaga mwili zikiendelea, Ofisa Habari KKKT Dayosisi ya Mwanga, Deodati Mushi amesema taratibu za kutoa heshima za mwisho zitaendelea na saa 9:00 alasiri itafanyika ibada fupi na baadhi ya waombolezaji na viongozi watapata fursa ya kutoa salamu za rambirambi.
“Kwa hapa kanisani, ratiba iliyopo kwa leo ni ibada, watu kutoa heshima za mwisho na baadhi ya waumini, waombolezaji na viongozi watapata fursa ya kutoa salamu za rambirambi,” amesema.
Amesema mwili wa Askofu Sendoro utalala kanisani hapo na kesho Jumanne Septemba 17, 2024 ibada ya maziko itaanza saa 4:00 asubuhi na itaongozwa na Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa na kuhudhuriwa na maaskofu mbalimbali wa kanisa hilo pamoja na viongozi wa dini na Serikali.