Mpina amvaa Bashe kivingine – Mwanahalisi Online

 

MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, amesema wananchi hawawezi kukaa kimya pale wanapocheleweshewa huduma za kijamii ikiwamo kuuziwa pembejeo feki, kwa kuogopa kuambiwa wanafanya siasa. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaan … (endelea).

Kauli ya Mpina imekuja siku chache baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kufanya ziara jimboni Kisesa na kuelezwa kwamba wamekubaliana kuweka tofauti zao pembeni, ili kuwaletea wananchi maendeleo na kumtaka Mpina asiingize siasa kwenye shughuli za maendeleo.

Jana Jumapili, Mpina alisema: “Leo hii, waziri wa Kilimo anataka kutuambia hivi, wananchi wakiuziwa mbegu feki, wakalalamika kwa wabunge wao, wabunge wao wakae kimya, eti kwa sababu wakiongea, watasema kwamba nyinyi mnaingilia kilimo ni wanasiasa. Wakiuziwa mbegu zilizooza, viongozi wasizungumze. Wakicheleweshewa mbegu, wasizungumze.”

Alisema kauli ya Bashe inawataka wananchi wakiuziwa pembejeo feki, wakae kimya na wakiona viongozi wa umma wanafanya ubadhirifu wasihoji.

“Eti diwani asizungumze, mbunge asizungumze, rais asizungumze; hayo ni sawa?” alihoji.
Aliwataka watendaji wa serikali wasiotaka kuingiliwa na wanasiasa, watoke kwenye ofisi za umma wanazozitumikia.

“Kama wewe hutaki kuingiliwa na mwanasiasa, achia ngazi nenda kakae nyumbani kwako kama utaona wanasiasa wamekuingilia…tutaendelea kuwadhibiti, tutaendelea kuwakagua kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikishindikana kule tutawapeleka mahakamani.”

Alisema wanasiasa wapo kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, diwani, mbunge hadi rais na viongozi wa vyama, ambao wapo kwa mujibu wa sheria na wamepewa jukumu la kuisimamia serikali.

Alisema mtendaji yeyote wa serikali ajiandae kukutana na mkono wa mwanasiasa, akieleza kuwa wanaowaogopa wawakilishi wa wananchi, ni wale wasiosimamia haki wala sheria kwenye maeneo wanayoyaongoza.

Aidha, alisisitiza kwamba majukumu ya wanasiasa yameainishwa na kwamba hakuna namna mbunge au diwani, anaweza kumzuia Waziri yeyote kufanya kazi yake.

“Yaani unataka mwananchi amekanyagwa na tembo huko, tuende tukakushangilie bungeni, kwa kuogopa kwamba tukikuhoji tutasemwa sisi ni wanasiasa. Nataka nipeleke salamu hizi kwamba watendaji wa serikali wawaheshimu viongozi wa kuchaguliwa na wasifikiri wamepatikana kwa bahati mbaya,” alisema.

Mpina na Bashe wameonekana kutofautiana ndani na nje ya Bunge, kiasi cha Mpina kusimamishwa kuhudhuria vikao 15 vya Bunge, kwa kile kilichoelezwa ni kukiuka kanuni alipomtuhumu waziri Bashe kwa kukiuka utaratibu wakati wa utoaji wa vibali vya kuagiza sukari.

About The Author

Related Posts