Geita/Dar. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limeungana na wadau wengine kusisitiza uchunguzi huru dhidi ya matukio ya utekaji na mauaji ya raia.
Kauli ya Bakwata inakuja wakati wadau wengine wakiwemo wa haki za binadamu, wanasiasa na viongozi wa dini wakisisitiza kufanyika kwa uchunguzi huru, ili kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo.
Msisitizo huo wa wadau, asasi za kiraia na wanasiasa hasa wa upinzani, unatokana na mfululizo wa kuripotiwa kwa kupotea, kutekwa na kuuawa kwa raia.
Hali hiyo inatokana na kile kilichotokea Septemba 6, 2024 kwa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao aliyetekwa na wasiojulikana akiwa kwenye basi la Tashriff, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam na siku moja baadaye mwili wake ulikutwa umetupwa Ununio, Dar es Salaam akiwa ameuawa.
Leo Jumatatu, Septemba 16, 2024 akitoa salamu za Bakwata katika Baraza la Maulid inayofanyika kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), mkoani Geita, Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma amegusia suala hilo.
Mgeni rasmi kwenye baraza hilo ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Mruma amesema licha ya Tanzania kusifiwa kwa amani kwa muda mrefu, lakini hivi karibuni kumetokea matukio yanayoivunja, ikiwemo kutekwa kwa watu na kuuawa.
Ameeleza Bakwata inaungana na Rais Samia kulaani vitendo hivyo na wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi huru bila kufanya upendeleo wala kumkandamiza mtu na badala yake haki itendeke bila kujali itikadi ya wanaofanya unyama huo katika jamii.
“Vyombo vifanye uchunguzi huru, mtafute ufumbuzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, tunaomba wananchi muwe mabalozi wazuri wa kulinda na kutunza amani yetu na msikubali kutumiwa na yeyote kuvuruga amani ya nchi.
“Viende mbali zaidi na kujua dhamira yao ni nini, ili kutafuta ufumbuzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amewasihi wanaofanya uchunguzi huo kutofanya upendeleo au kumkandamiza yeyote, bali haki itendeke bila kujali itikadi za wanaofanya unyama huo.
“Tunaomba wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kutunza amani yetu na kutokubali kutumika na yeyote kwa maslahi binafsi katika kuvuruga amani yetu,” ameeleza.
Bakwata anatoa maelezo hayo sawia na yaliyoelezwa jana Jumapili Septemba 15 Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lililolaani vitendo hivyo likisema:“Sisi maaskofu hatuamini kama makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu ya ulinzi na usalama.
“Hivyo tunaviomba vyombo kutimiza wajibu wake, ili kurudisha heshima yetu ya misingi ya udugu na amani.”
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir akimkaribisha Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka Waislamu kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa, huku wakiweka elimu mbele na kuilinda amani ya nchi bila kuvuruga amani ya mtu.