Mahakama ilivyohitimisha mgogoro Profesa Assad kuteuliwa msuluhishi

Dar/Arusha.  Mahakama ya Rufani imemaliza mgogoro wa uteuzi wa aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kusuluhisha mgogoro baina ya kampuni ya Oilcom Tanzania Limited dhidi ya Oryx Oil company Limited na Oryx Energies SA.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa iliyokatwa na kampuni za Oryx Oil na Oryx Energies dhidi ya kampuni ya Oilcom, zikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoridhia uteuzi wa Profesa Assad.

Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa hiyo ya madai namba 47/2024, kutokana na pingamizi la awali lililowekwa na kampuni ya Oilcom, dhidi ya rufaa hiyo baada ya kukubaliana na sababu moja pekee kati ya nne za pingamizi la awali la Oilcom.

Sababu hiyo pekee ya pingamizi ambayo Mahakama imekubaliana nayo ni kwamba rufaa hiyo inatokana na uamuzi mdogo ambao haupaswi kukatiwa rufaa, kwani hauamui hatima ya haki za msingi za wadaawa katika mgogoro.

Uamuzi huo umetolewa Septemba 12, 2024 na jopo la majaji watatu—Ferdinand Wambali (kiongozi wa jopo), Lilian Mashaka na Benhajj Masoud katika kikao chake ilichoketi jijini Dar es Salaam kusikiliza pingamizi hilo kabla ya rufaa ya msingi.

Uamuzi huo Mahakama ya Rufani, imekata mzizi wa fitina na kuhitimisha mvutano wa muda mrefu baina ya kampuni hizo kuhusiana na uhalali wa uteuzi wa Profesa Assad.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hiyo katika hoja zake kuhusiana na sababu ya pingamizi iliyoamua rufaa hiyo, Wakili wa Oilcom, Thobias Laizer alidai rufaa hiyo haikuwa na uhalali.

Alifafanua uamuzi wa Mahakama Kuu uliokatiwa rufaa hiyo ni uamuzi mdogo ambao haukuamua na kuhitimisha masuala ya msingi ya mgogoro wa wadaawa, bali ulishughulikia uhalali wa wajumbe wa baraza la usuluhishi.

Hivyo, alidai rufaa hiyo haina uhalali kwa kifungu cha 5(2) (d) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa (AJA) kinazuia rufaa dhidi ya uamuzi au amri za Mahakama Kuu zisizoamua haki za msingi za wadaawa.

Katika kuunga mkono hoja yake hiyo aliirejesha Mahakama katika mashauri mengine mbalimbali iliyokwishayaamua kuhusu msimamo huo wa kisheria.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Oryx, Gasper Nyika alidai rufaa hiyo haibatilishwi na kifungu cha 5(2) (d) cha AJA kwa sababu shauri la warufani Mahakama Kuu (kupinga uteuzi wa Profesa Assad) lilifunguliwa chini ya vifungu vya 27 na 28 vya Sheria ya Usuluhishi.

Hivyo alidai baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali shauri hilo, hakukuwa na suala lolote lililobakia mbele yake kuhusiana na kuondolewa au vinginevyo kwa msuluhishi, kuhitaji kutumia kifungu cha 5 (2) (d) cha AJA kuhusu uhalali wa rufaa hiyo mahakamani hapo.

Wakili Nyika alisisitiza masharti ya kifungu cha 5(2) (d) cha AJA yanazuia rufaa dhidi ya mashauri yaliyoko Mahakama Kuu na si mashauri ya kutoka baraza la usuluhishi.

Alidai uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri la madai namba 138/2022 wa kulitupilia mbali umefunga milango ya kutafuta haki kuhusiana na kutokuwa na upande kwa msuluhishi, hivyo warufani hawawezi kuzungumzia tena hoja hiyo baada ya tuzo kutolewa.

Mahakama katika uamuzi wake ulioandikwa na Jaji Wambali kwa niaba ya jopo hilo, huku ikinukuu kifungu cha 5(2) (d) cha AJA, imesema kinakataza rufaa dhidi ya amri au uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu.

Mahakama imesema hakuna shaka kwamba shauri la msingi namba 138/2022, lililokatiwa rufaa lilitokana na shauri la usuluhishi mbele ya baraza la usuluhishi ambalo lina mamlaka ya kuamua mgogoro huo wa wahusika kuhusiana na madai ya ukiukaji wa mkataba.

Hata hivyo, imesema masharti ya kifungu cha 27(4) (b), kilichotumiwa na warufani katika kufungua shauri la msingi hakikusudiwa kumvisha haki zaidi ya kukata rufaa mdaawa asiyeridhika na uamuzi wa Mahakama Kuu kukataa au kukubali maombi ya kumuondoa msuluhishi.

“Kwa kuzingatia uamuzi wa Mahakama Kuu, tuna maoni kwamba ingawa hakuna kilichosalia kuhusu suala la kumwondoa msuluhishi, haukufungia mlango wadaawa kurejea baraza la usuluhishi kushiriki madai yao ya msingi yanayohusu uamuzi wa mzozo wao hadi kutolewa tuzo ya mwisho,” amesema Jaji Wambali.

Pia Mahakama hiyo imesema uamuzi wa Mahakama Kuu haujafunga mlango kwa warufani kufika katika Mahakama hiyohiyo kupinga tuzo ya mwisho kwa mujibu wa kifungu cha 74 (1) (a) na (b) cha Sheria ya Usuluhishi.

Imesisitiza chini ya vifungu vya 75 na76 ya Sheria ya Usuluhishi, upande usioridhika unaruhusiwa kupinga tuzo hiyo Mahakama Kuu kama kutakuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na vilevile upande usioridhika unaweza kukata rufaa mahakamani hapo chini ya kifungu cha 6.

Mahakama baada ya kuchambua vifungu mbalimbali vya Sheria ya Usuluhishi, mazingira, asili ya shauri la usuluhishi lililoko baraza la usuluhishi na ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliokatiwa rufaa imehitimisha kuwa uamuzi huo unaangukia katika masharti ya kifungu cha 5(2) (d) cha AJA.

Hivyo imesema haiwezi kuhitimisha kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ambao ndio msingi wa rufaa hiyo uliamua hatima ya haki za wadaawa na kwamba pingamizi la awali dhidi ya rufaa hiyo limekubaliwa.

“Kwa mwisho huu, kwa kuzingatia uamuzi tulioufikia, hatuoni haja ya kuendelea na uamuzi wa sababu nyingine tatu za pingamizi la awali,” amesema Jaji Wambali katika uamuzi huo na kuhitimisha:

“Hatimaye tunaona kuwa rufaa hii haistahili, kutokana na kukiuka masharti ya kifungu cha 5(2) (d) cha AJA. Kwa hiyo tunaitipilia mbali kwa gharama (upande ulioshindwa kuulipa upande ulioshinda gharama za kuendesha shauri hilo).”

Historia ya mgogoro uteuzi wa Profesa Assad

Novemba 18 na Desemba 5, 2016, kampuni hizo ziliingia mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa shughuli za kibiashara.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo mgogoro au tofauti baina yao utawasilishwa katika jukwaa la usuluhishi linaoundwa na wasuluhishi watatu, huku kila upande ukiwa na haki ya kuchagua msuluhishi wake na yule anayechaguliwa na pande zote kuwa mwenyekiti.

Hata hivyo, baadaye katika utekelezaji makubaluano hayo kampuni hizo zilijikuta katika mgogoro uliotokana na kutokukubaliana katika tafsiri ya baadhi ya vifungu vya makubaliano zilizoingia, baada ya Oilcom kuzilalamikia Oryx kukiuka vigezo na masharti ya kibiashara walivyokubaliana.

Hivyo, katika kufikia suluhu ya mgogoro huo kampuni hizo zilikwenda kwenye baraza la usuluhishi kwa mujibu wa mkataba huo na wasuluhishi watatu walioteuliwa na pande zote, akiwemo Profesa Assad aliyekuwa na Oilcom.

Kabla ya Mwenendo wa usuluhishi kuanza, kampuni za Oryx zilimkataa Profesa Assad kutokana na taarifa zilizoko katika hati ya maelezo yake binafsi (curriculum Vitae – CV), kuwa Machi 2006 alifanya kazi na kampuni ya Oilcom akiwa mshauri pekee katika mpango wa biashara.

Kwa taarifa hizo kampuni hizo zilihisi kwamba taarifa hizo ambazo hazikuwa zimewekwa wazi kwao ziliibua mashaka kuhusu uhuru wake, akikaa kama msuluhishi katika mgogoro wao. 

Hivyo, Machi 11, 2022 zilimwandikia barua Profesa Assad zikimtaka ajiondoe, lakini Profesa Assad aligoma.

Katika majibu yake kupitia barua yake ya Machi 16, 2022 alikana kufanya kazi na kampuni ya Oilcom katika wakati wowote, alidai mradi huo ulikuwa ukiendeshwa kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilala ambayo ndio mteja aliyemhusisha.

Hivyo alidai wakati wote huo hakuwahi kuwa na mawasiliano wala kukutana na mtu yeyote kutoka katika menejimenti ya kampuni ya Oilcom na kwamba yeye yuko huru na haoni mgongano wa maslahi kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

Kutokana na msimamo huo wa Profesa Assad, kampuni hizo za Oryx zilikwenda kumpinga mahakamani na zilifungua shauri la maombi namba 138 la mwaka 2022.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Mustapha Ismail Oktoba 18, 2022, ilitupilia mbali shauri hilo.

Jaji Ismail alitipilia mbali shauri hilo pamoja na mambo mengine akieleza kuwa hisia za upendeleo, zilizodaiwa na Oryx ni za kimtazamo zaidi kuliko uhalisia, ambazo hazijafaulu katika kiwango cha juu cha ufahamu au tuhuma zenye mashiko.

“Uamuzi katika shauri la usuluhishi ni wa wasuluhishi walio wengi. Msuluhishi mmoja pekee hawezi kuwa na ushawishi, kuyumbisha uamuzi wa jopo”, alisema Jaji Ismail.

Kampuni za Oryx hazikuridhika na uamuzi huo ndipo zikakata rufaa hiyo Mahakama ya Rufani kuupinga, kisha Oilcom nayo ikaibua pingamizi liliiondoa rufaa hiyo mahakamani.

Related Posts