Mabadiliko ya kiteknolojia yanavyoathiri ukuaji wa watoto

Geita. Mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi, utandawazi pamoja na kupungua kwa mshikamano wa kijamii, vimetajwa kuwa chanzo cha kukosekana kwa misingi imara ya maadili, upendo na nidhamu kwa watoto.

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema hayo jana Septemba 15, 2024 wakati wa mahafali ya 12 ya Shule ya Msingi Waja iliyopo mkoani Geita.

Gombati amesema mazingira mapya yanayojumuisha maendeleo ya haraka ya teknolojia na mabadiliko katika sekta ya kiuchumi, yamechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika mitindo ya maisha ya familia na jamii kwa ujumla.

Amesema hali hiyo inachangia kupungua kwa muda wa pamoja wa familia, kupungua kwa mawasiliano ya karibu na kupotea kwa usimamizi wa karibu katika malezi ya watoto.

“Mabadiliko haya yanayoletwa na utandawazi, pia yameathiri njia za mawasiliano kwa watoto, sasa wanapata maelekezo na maadili kutoka kwa vyanzo vingi vya nje ya familia na mara nyingi visivyo na thamani sawa na yale yanayokubalika katika jamii na kusababisha kupungua kwa nidhamu na uelewa wa maadili ya kimsingi,” amesema Gombati.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wazazi kuzingatia umuhimu wa kuweka misingi thabiti ya maadili na nidhamu kwa watoto, licha ya changamoto za teknolojia na kiuchumi zilizopo.

Amesema ili kuhakikisha ukuaji bora wa watoto, ni muhimu familia kuimarisha mshikamano na usimamizi wa malezi, huku wakichangamkia fursa za elimu zinazotolewa na teknolojia kwa njia yenye manufaa.

“Wazazi imarisheni misingi ya malezi ya watoto, hakikisheni kuwa pamoja na teknolojia na mabadiliko mengine yanatumika kwa njia itakayoleta faida katika ukuaji wa watoto,” amesema Gombati.

Mkurugenzi wa Shule za Waja, Chacha Wambura amewataka wazazi kutowapa simu watoto wao kipindi hiki cha likizo ya kusubiri kuanza masomo ya sekondari na badala yake watumie muda huo kuwapa maadili mema pamoja na kuwafundisha kazi za nyumbani.

Akizungumza kwa niaba ya ya wazazi wenye watoto waliohitimu darasa la saba, Godfrey Noel amesisitiza umuhimu wa kubadilisha mifumo ya elimu katika shule za msingi na sekondari, ili kuandaa wanafunzi kwa ujasiriamali badala ya kutegemea ajira pekee.

Amesema kwa kufanya hivyo kutaongeza uwezo wa vijana kujiajiri na kukuza vipaji vyao kwa manufaa ya Taifa.

“Ni muhimu shule zianzishe programu maalumu za ujasiriamali na kuwapa wanafunzi mafunzo ya vitendo kuhusu biashara, usimamizi wa fedha, na uendeshaji wa miradi, hii itasaidia wanafunzi kuwa na mtazamo wa biashara na kujifunza jinsi ya kubuni mawazo mapya, badala ya kuwa na mawazo ya kutegemea ajira pekee,” amesema Noel.

Hata hivyo, ameishauri Serikali kuwapatia walimu mafunzo ya ziada juu ya mbinu za kufundisha ujasiriamali na namna ya kubaini na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Related Posts