Chomelo aisikilizia Konya | Mwanaspoti

MCHEZAJI wa timu ya Konya Amputee ya Uturuki na timu ya taifa ya walemavu ya Tanzania ‘Tembo Warriors’, Ramadhan Chomelo amesema sio muda mzuri wa kuzungumzia mkataba wake na klabu hiyo kwani bado ligi haijaanza.

Chomelo alisaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2022 uliotamatika msimu huu.

Akizungumzia juu ya hatma yake kikosini hapo, Chomelo alisema anafahamu hilo lakini kwa sasa yupo Tanzania mapumzikoni hivyo kwake sio muda sahihi ingawa mpira ni biashara lolote linaweza kutokea.

“Unajua haya mambo ya mikataba ni siri baina ya klabu na mchezaji, msimu bado haujaanza hivyo siwezi kuzungumza chochote tusubiri kwanza, hata hivyo ligi inaanza Oktoba tutajua,” alisema Chomelo.

Kuhusu kiwango chake msimu huu alisema hakufanikiwa kumaliza ligi kutokana na majukumu ya timu ya taifa ‘Tembo Warriors’ lakini ulikuwa msimu bora kwake.

“Utofauti wa Ligi ya Tanzania na Uturuki ni ndogo, wenzetu wana klabu nyingi lakini sisi klabu shiriki ni chache lakini kwenye ushindani tunaendana.”

Msimu wake wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na kutoa asisti 16 huku msimu uliopita 2023/24 akicheza mechi 21 na kufunga mabao manne na kutoa asisti tisa.

Related Posts