Pacome arudi kikosini Yanga ikiivaa Tabora United

HATIMAYE kiungo wa Yanga Pacome Zouzoua Leo anarudi uwanjani kwa mara ya kwanza tangu kuumia na kuzusha taharuki kubwa.

Kwenye kikosi cha Yanga kitakachocheza mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Tabora United kiungo huyo ni kati ya wachezaji 18 watakaocheza mchezo huo.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa kiungo huyo hataanza kwenye kikosi cha kwanza cha wachezaji 11 badala yake atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa benchi.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi anataka kumpa muda wa dakika chache kiungo huyo kucheza kipindi cha pili baada ya kupona sawasawa jeraha la goti la mguu wa kushoto.

Kiungo huyo Muivory Coast tangu alipoumia kwenye mchezo dhidi ya Azam FC wa Ligi Kuu Bara alioucheza kwa dakika 10 pekee amekuwa nje na kukosa jumla ya mechi saba.

Wakati akiwa nje taharuki kubwa ilizuka kwa kiungo huyo akidaiwa kuwa na matatizo mengine kwenye usajili wake mbali na majeruhi, sintofahamu ambayo hata hivyo ilizimwa na uongozi wa Yanga ukisisitiza kwamba ni majeraha pekee yaliyomuweka nje Pacome.

Related Posts