TIMU ya KenGold imeendeleza mwenendo mbaya wa matokeo ya Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuchapwa bao 1-0 na KMC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Mwenge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kichapo cha tatu mfululizo kwa kikosi hicho.
Bao la KMC limefungwa na nyota wa kikosi hicho, Redemtus Mussa katika dakika ya 15 tu ya mchezo huo baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa KenGold, Castor Mhagama, na hivyo kufikisha bao lake la pili msimu huu katika Ligi Kuu Bara na timu hiyo.
Redemtus alifunga pia katika mchezo uliopita ambao KMC ilichapwa mabao 2-1 na Singida Black Stars kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida Septemba 12, mwaka huu.
KenGold inayonolewa na kocha Fikiri Elias inaendelea kuteseka katika Ligi Kuu Bara kwani timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kwa mara yake ya kwanza baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship, haijaonja ladha ya ushindi.
Timu hiyo ilianza ligi kwa kichapo cha mabao 3-1, ikiwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, kisha kuchapwa ugenini 2-1, na Fountain Gate kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati, mechi ikipigwa Septemba 11.
Kwa upande wa KMC inavuna pointi tatu za kwanza kwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara baada ya kuanza sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Coastal Union Agosti 29, kwenye Uwanja wa KMC, kisha kuchapwa ugenini 2-1 na Singida Black Stars, Septemba 12.
Ushindi kwa KMC unakifanya kikosi hicho kufikisha pointi nne na kushika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku kwa upande wa KenGold ikishika nafasi ya 14 bila ya pointi yoyote, baada ya kila mmoja kucheza michezo yake mitatu.
Hadi sasa Singida Black Stars ndio inayoongoza Ligi Kuu Bara baada ya kushinda michezo yote mitatu na kukusanya jumla ya pointi tisa, ikifuatiwa na ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’ Mashujaa ya Kigoma inayoshika nafasi ya pili na pointi zake saba.
Fountain Gate inafuatia ikiwa nafasi ya tatu na pointi saba pia kama ilivyo kwa Tabora United inayoshika ya nne ila timu hizo zote zikicheza michezo minne hadi sasa ya Ligi Kuu Bara, zikiwa ndizo zinazoongoza tofauti na klabu nyingine.