Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amesema watafanya uchambuzi wa haraka kubaini maeneo mengine yaliyoachwa na Serikali katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Kwa mujibu wa Semu, kwa haraka haraka wamebaini kata tatu za Ulyankuku (Tabora) Katumba na Mishamo (Katavi) kutotambuliwa katika Tangazo la Mipaka ya Vijiji, 12,333, vitongoji 64,274 na Mitaa 4,269 vitakavyohusishwa katika uchaguzi huo.
Mapema leo Jumatatu Septemba 16, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametoa tangazo la amri na notisi ya mgawanyo wa maeneo ya kiutawala katika serikali za mitaa.
Amri ya mgawanyo wa maeneo ya utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) (Tangazo la Serikali Na. 796 la mwaka 2024) imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287.
Kuhusu notisi ya mgawanyo wa maeneo ya utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Tangazo la Serikali Na. 797 la mwaka 2024) imetolewa kwa mujibu wa vifungu vya 16(1) na 18(1) vya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.
Akiwahutubia wananchi wa Lushoto mkoani Tanga katika mwendelezo wa ziara ya viongozi wakuu wa chama hicho, waliojigawanya kikanda, Semu amesema wameliona tangazo hilo na katika siku chache zijazo watakaa kufanya uchambuzi wa kina.
“Kwa haraka haraka tumeona kata za Ulyankulu, Katumba na Mishamo kutotambuliwa kwenye mchakato huu uliotangazwa, kata hizi zilipewa hadhi ya kuwa maeneo halali ya wananchi baada ya kutoka kuwa makazi ya ukimbizi.
“Kwa mara ya kwanza Watanzania wapya walishiriki uchaguzi wa serikali mwaka 2015 na 2020, lakini Serikali imeendelea kuwanyima haki ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,” amedai Semu.
Semu amesema ACT- Wazalendo, ilikuwa na shauku ya kuona Serikali kama itazingatia kilio cha Watanzania wa Ulyankulu, Katumba na Mashimo, lakini kwa tangazo lililotolewa na Tamisemi limeendelea kuwaacha na kilio.
“Niwahakikishie Watanzania timu yetu makini ya chama itafanya uchambuzi haraka kuona kama kuna vijiji, mitaa na vitongoji vingine vimeachwa kufuatia tangazo hilo, kisha tutautaarifu umma,” amesema Semu.
Katika ziara hiyo, Semu amewahimiza Watanzania na wananchi wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi Novemba 27 mwaka huu, kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kutumia haki yao ya kikatibu ya kuchagua na kuchaguliwa.
“Mjitokeze kupiga kura, msitishike na vitisho vya aina yoyote, nenda mkakichagueni ACT- Wazalendo, ndiyo chama mbadala kwa sasa kitakachowaletea maendeleo,” amesema Semu.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Pwani hususan wilaya za Mafia, Kibiti, Mkuranga na Rufiji kwamba chama hicho kitakuwa mstari wa mbele kuzisemea kero zinazowakabili, ikiwemo ya migogoro ya ardhi.
“Niwaambie wananchi wa Mkoa wa Pwani, mmepata mtetezi wa kero zinazowakabili, tutahakikisha tunazisemea ili zipatiwe ufumbuzi wa kuduma,” amesema Ado wakati akiwahutubia wananchi wa wilaya hizo kwa nyakati tofauti.