Dar es Salaam. Wajasiriamali wadogo wadogo nchini wamehakikishiwa kuendelea kupatiwa ufumbuzi wa tatizo la mitaji ya kibiashara katika kuingiza sokoni bidhaa zao zenye ubunifu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kukidhi mageuzi ya sayansi na teknolojia.
Hakikisho hilo, limetolewa na Benki ya Kibiashara ya DCB, wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Mwaka wa Wanahisa wa taasisi hiyo huku ikieleza dhamira yake ni ni kusaidia miradi endelevu ya kupunguza umasikini.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo,Sabasaba Moshingi amesema benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wanaopata changamoto za kupata huduma hizo.
“Pia tumeendelea kufanya vizuri katika mikopo ya watu binafsi na vikundi vya wajasiriamali huku tukiendelea kuboresha mikopo hiyo ili iendane na mahitaji yao halisi,” amesema
Katika maelezo yake amebainisha kwa kipindi cha miaka 22 tangu kuanzishwa kwa tasisi hiyo wanajivunia kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh741bilioni iliyowanufaisha zaidi ya watanzania 420,000.
Mkurugenzi huyo amesema moja ya hatua walizochukua wakati wakiandika upya historia ya taasisi hiyo ni kuzindua mpango wa mkakati wa miaka mitano ulioanza tangu 2023 hadi 2028 lengo kuongeza mtaji kutoka Sh16 bilioni hadi Sh61bilioni.
“Tunafanya hivi ilikuendana na takwa la kisheria la Benki Kuu ya Tanzania (BoT),lakini pia kukuza amana za benki, kukuza idadi ya matawi, kukuza mikopo na kupunguza kiwango cha mikopo chechefu (NPL) kutoka kiwango cha 4.7 ili kuwa chini ya asilimia 4.4,” amesema.
Moshingi amesema wanatoa mikopo ya wanawake, na wanafanya vizuri katika mikopo mingine ya vikundi, mikopo ya nyumba, mikopo ya wafanyakazi hususan walimu, mikopo ya guta, pikipiki na bajaji na mingineyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha DCB,Siriaki Surumbu amesema benki imeendelea kukuza mapato ikijikita katika shughuli za utoaji mikopo yenye ubora hasa kwa vikundi maalum vya wanawake na wajasiliamali.
Awali katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Zawadia Nanyaro amesema malengo yao huduma za tasisi hizo ziwe zinapatikana nchi nzima.
Vilevile amesema wanaendelea na mpango wao wa kukuza amana za wateja kufikia nusu trilioni, faida jumuishi kuwa Sh37 bilioni, kuimarika kwa ufanisi wa benki hadi asilimia 54 kwa kulinganisha gharama za uendeshaji wa benki na mapato yake.
“Nipende kutoa shukurani kwa serikali kuweka mazingira yanayosaidia sekta ya fedha kufanya biashara katika mazingira bora na wezeshi.
“lakini pia kwa kuona umuhimu wa kushirikisha sekta binafasi katika miradi ya kimkakati inayoendelea kwa mafanikio katika sehemu mbalimbali nchini,” amesema Nanyaro.