‘Usioe kama unakwepa kulipa kodi, utaipa mzigo Serikali’

Unguja. Ikiwa wewe ni kijana ambaye hujaoa au kuolewa kama unakwepa kulipa kodi, usioe. Imeelezwa.

 Meya wa Baraza la Mji Kaskazini A Unguja, Machano Fadhil Machano ametoa kauli hiyo jana Septemba 15, 2024 wakati akifungua mkutano wa elimu ya mabadiliko ya kodi ya sheria za kodi kwa walipakodi ulioandaliwa na Mamlaka ya Kulipa Kodi Zanzibar (ZRA).

 “Lazima kwa kila kijana awajibike katika suala la kulipa kodi, kabla hajaingia katika ndoa kwa kuwa kizazi kinachopatikana kinatarajia kodi zinazokusanywa, kama wewe hulipi kodi basi hupaswi pia hata kuoa,” amesema.

 Msingi wa kauli ya Meya Machano inatokana na ukweli kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake bila malipo, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kufahamu Serikali inatumia gharama kubwa kugharamia mambo na kinachotumiwa kinatokana na kodi zinazolipwa.

 Baadhi ya huduma zinazotolewa bure na SMZ ni afya, maji na elimu.

 “Iwapo Wazanzibari wanahitaji kuwa na Serikali itakayoweza kuhudumia vizazi na jamii ya Wazanzibari kwa ujumla, suala la kodi linapaswa kupewa kipaumbele kabla vijana hawajaamua kuingia katika ndoa,” amesema.

 Wakizungumza kuhusu jambo hilo, baadhi ya vijana wamekuwa na mtazamo tofauti wakisema kulipa kodi ni muhimu, lakini kuoa pia ni muhimu.

 “Hakika kulipa kodi ni muhimu tunatakiwa ulipa zaidi, lakini na kuoa ni muhimu, kwa hiyo haya mambo yote yanatakiwa kufanyika,” amesema Abdulla Khamis, mkazi wa Banda maiti

 Meneja wa Kodi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hanii Mohamed Khamis amewataka wafanyabiashara kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZRA, ili kuifanya kazi ya ukusanyaji wa mapato na ulipaji kodi iwe rahisi kwa pande zote mbili.

 Amesema wafanyabiashara wana wajibu wa kuendelea kufanya biashara kwa kufuata misingi ya sheria za kodi, ikiwemo kuwasilisha malipo kwa wakati sambamba na kutoa risiti za kielektroniki kila wanapofanya mauzo.

 Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi ZRA, Makame Khamis Moh’d amesema marekebisho ya sheria za kodi pamoja na mambo mengine yamezingatia uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha uwekezaji katika uchumi wa buluu.

 Miongoni mwa sheria zinazosimamiwa na ZRA ambazo zimefanyiwa marekebisho kwa mwaka huu ni pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Kodi ya Majengo pamoja na sheria ya ushuru wa bidhaa.

Wakati huohuo Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed wameonya watumishi wa mamlaka hiyo kusimamia maadili ya utumishi na kujiepusha na vishawishi vya kupokea rushwa, jambo litakaloathiri utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato.

 Pia amewataka kusimamia haki bila kumuonea wala kumpendela mtu, hivyo wanatakiwa kuzisoma na kuzielewa sheria za kodi wanazozisimamia watendaji hao.

 “Lazima watendaji kuzingatia maadili na kutenda haki, tuzisome sheria zinazotuongoza hili litatusaidia kutojiingiza kwenye vitendo vya rushwa na kuisaidia Serikali kukusanya mapato makubwa,” amesema Said alipozungumza na watumishi hao ChakeChake, Mkoa wa Kusini Pemba.

 Mkurugenzi Ofisi ya ZRA Pemba, Jamal Hassan Jamal amesema Ofisi ya ZRA Pemba kwa mwaka huu wa fedha imekadiriwa kukusanya Sh47.971 bilioni na kwa miezi miwili ya mwanzo wa mwaka imefanikiwa kukusanya Sh8 bilioni, sawa na wastani wa asilimia 103.84 ya makadirio.

Related Posts