LONDON, ENGLAND. LIVERPOOL na West Ham United zimetolewa katika michuano ya Europa League, baada ya kushindwa kupindua meza katika michezo ya mkondo wa pili.
Liverpool ambayo ilichapwa bao 3-0 na Atalanta, Alhamisi wiki iliyopita uwanjani Anfield imeibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano, lakini haujaisaidia.
Bao hilo la Liverpool ambalo limefungwa dakika ya saba kwa penalti ya Mohamed Salah, liliibua matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo walioamini kwamba wanaweza kumaliza hata kwa sare katika dakika 90 kisha wakashinda mechi katika dakika 30 za ziada au penalti.
Lakini hilo halikutimia kwani Atalanta ilionekana kulinda vyema lango lake, na nafasi chache ambazo Liverpool ilizipata ilishindwa kuzitumia.
West Ham ilikuwa ikiumana na Bayer Leverkusen, mabingwa wa Bundesliga msimu huu, mechi ikamalizika kwa sare ya bao 1-1.
Leverkusen ilifanikiwa kusonga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 kwani mechi ya mkondo wa kwanza nchini Ujerumani ilishinda bao 2-0.
Katika sare ya 1-1, West Ham ndio ilikuwa yakwanza kupata bao dakika ya 13 kupitia kwa Antonio, wakati Leverkusen ikisawazisha dakika ya 89 kwa bao la Jeremie Frimpong.
Kutoka kwa timu hizo kunaifanya England kubakisha timu moja tu katika michuano ya kimataifa ambayo ni Aston Villa iliyopo nusu fainali ya Uefa Europa Conference League ikitarajia kucheza na Olympiacos Mei 02.
Timu nyingine zilizotolewa robo fainali katika Europa League ni AC Milan na Benfica. Katika hatua ya nusu, Marseille itakutana na Atalanta kisha Roma itacheza dhidi ya Leverkusen, mechi za mkondo wa kwanza zitapigwa Mei 02 na marudiano Mei 09.